Mabomu ya vishada ya muungano vamizi katika vita vya Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia yanayovurumishwa kwa wananchi wasio na hatia hadi kufikia mwaka jana wa 2021 yameuwa raia karibu elfu nne wa nchi hiyo.
Taasisi za Umoja wa Mataifa likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) zimetahadharisha mara kadhaa kuwa wananchi wa Yemen wanakabiliwa na njaa na maafa makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika karne moja iliyopita kutokana na mashambulizi ya nchi vamizi huko Yemen.
Televisheni ya al Aalam imeripoti kuwa, kitengo cha kutegua mabomu ya kutegwa ardhini cha Sana’a kimethibitisha kuwa, zaidi ya raia 3,841 wa Yemen wameuawa na kujeruhiwa kwa mabomu ya vishada ya muungano vamizi wa Saudia kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka jana wa 2021. IKitengo hicho pia kimetangaza kuwa idadi kubwa ya waliopoteza maisha na kujeruhiwa kwa mabomu hayo ya vishada ya muungano vamizi huko Yemen ni wanawake na watoto.
Wakati huo huo kitengo hicho cha kutegua mabomu ya kutegwa ardhini cha Yemen kimetangaza kuwa: Katika kipindi chote hicho, zaidi ya aina 15 za mabomu ya vishada yalitumiwa katika mikoa 15 na maeneo 70 nchini Yemen. Mabomu hayo ya vishada na silaha zilizopigwa marufuku zimetumiwa na muungano vamizi wa Saudia kuwasababishia masaibu mbalimbali na kumwaga damu za watu wa Yemen.