Takwa la Rais wa Ufaransa kwa Ulaya la kujiepusha na utegemezi wa kijeshi kwa Marekani

Jumatatu ya jana tarehe 19 Juni, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alizitaka nchi za Ulaya kutafuta uhuru zaidi katika ulinzi wa anga zao na kuacha kuwa tegemezi kupita kiasi kwa Marekani.

Akihutubia mwishoni mwa mkutano wa Paris ambapo mawaziri wa ulinzi na wawakilishi wengine wa nchi 20 za Ulaya walihudhuria, Macron alielezea mtazamo wake kuhusiana na wazo la kulindwa anga ya Ulaya na madola ya Ulaya yenyewe.

Mkutano huu ulihudhuriwa na Ujerumani, Uingereza na Sweden, pamoja na majirani wa Ukraine kama vile Poland, Slovakia, Hungary na Romania, pamoja na wawakilishi wa NATO na Umoja wa Ulaya. Macron aliwataka watengenezaji wa zana na vifaa vya ulinzi wa Ulaya kuunda mifumo huru ya kijeshi na kuizalisha kwa ajili ya bara hilo.

Ufaransa imekosoa waziwazi mpango wa Ujerumani wa kuboresha uwezo wa ulinzi wa anga wa Ulaya. Mpango huo unaoitwa European Sky Shield, ambao ulizinduliwa mwishoni mwa mwaka jana (2023), unajumuisha nchi 17 za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Uingereza, lakini Ufaransa haishiriki katika hilo.

Mpango huu unatarajia kuunganishwa katika mifumo ya ulinzi wa anga na makombora ya Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO. Serikali ya Ufaransa inaamini kwamba, mpango huu hauhifadhi mamlaka ya Ulaya, kwa sababu vifaa hivyo kwa asilimia kubwa vitategemea zaidi sekta ya viwanda ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Takwa la Macron la kujiepusha Ulaya na suala la kuwa tegemezi wa kijeshi kwa Marekani linalingana na wazo na uoni wake jumla wa kudumishwa uhuru wa kimkakati wa Ulaya na kuwa na nafasi Ulaya katika medani ya kimataifa ukiwa mchezaji huru asiye na utegemezi wa Marekani wala China.

Baada ya kuzuru China mwezi Aprili 2023, Macron alitoa mwito wa uhuru wa kimkakati wa Ulaya kutoka kwa Marekani na kusema: Utegemezi wa Ulaya kwa Marekani katika uga wa silaha na nishati umeongezeka na kuwa mkubwa na kwamba, sasa umewadia wakati kwa Ulaya kujikita zaidi katika suala la kuimarisha sekta zake za ulinzi.

Katika miaka ya hivi karibuni, Rais wa Ufaransa amesisitiza mara kwa mara haja ya kuunda jeshi huru la Ulaya. Kabla ya hapo, Januari 2023, Emmanuel Macron, sambamba na kutoa mwito wa kupunguzwa utegemezi wa usalama na kiuchumi wa Ulaya kwa Marekani alisisitiza kwamba, Brussels inapaswa kusimama dhidi ya sera za serikali ya Marekani za kuunga mkono makampuni yake na kuanzisha mkakati wa kuijenga Ulaya.

Alitoa wito wa kutekelezwa kwa mkakati wa kiuchumi wa “kuijenga Ulaya” katika bara hilo kwa lengo la kuunga mkono mtandao wa viwanda wa Ulaya, kuanzisha nafasi za ajira na kuongeza nguvu ya ushindani kwa ajili ya kukabiliana na sera za Marekani.

Macron anasema: “Tunahitaji mkakati wa “Kujenga Ulaya” ili kuendana na maendeleo ya kimataifa na kuwa jibu kwa sera ya Marekani.” Mkakati wa kiuchumi wa “Kujenga Ulaya” uliopendekezwa na Macron kwa hakika ni mpango wa kukabiliana na sera za kiuchumi za Marekani ambayo inataka kulinda bidhaa zake za ndani dhidi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka Ulaya.

Rais wa Ufaransa ana wasiwasi sawa na huo katika uga wa kufuata na kuwa na utegemezi wa kijeshi wa Ulaya kwa Marekani. Licha ya Ulaya kuwa pamoja na Marekani katika vita vya Russia na Ukraine, Macron anaamini kuwa Ulaya inapaswa kuwa na uwezo huru wa kijeshi na kutokuwa tegemezi kwa Marekani, kama vile katika uwanja wa uzalishaji na utumiaji wa aina ya mifumo ya silaha inayohitajika kwa ajili ya kujilinda, hususan mifumo ya ulinzi wa anga na iliyo dhidi ya makombora.

Ukweli wa mambo ni kuwa, baada ya vita vya Ukraine, Berlin imetazama upya na kwa njia ya kimsingi sera zake za ulinzi, sio tu iliongeza sehemu ya gharama za kijeshi katika pato la Taifa bali ikiwa na lengo la kudhamini zana zake za kijeshi ilianza kununua ndege za kivita za F-35 za kizazi cha tano kutoka Marekani.

Hii ni katika hali ambayo, Ufaransa inasisitiza juu ya haja ya kuzalisha na kununua zana za kijeshi na aina zote za silaha kutoka ndani ya Ulaya. Suala hili hivi sasa limedhihirika katika upinzani wa Rais wa Ufaransa wa ununuzi wa zana za mfumo wa ulinzi wa anga kutoka Marekani na mshirika wake, utawala wa Kizayuni.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *