Kupamba moto vita vya Russia na Ukraine na kusambaa mgogoro wa kiuchumi katika akthari ya mataifa ya dunia, kumezifanya nchi za Kiafrika zitengwe na kutupwa mkono zaidi.
Hali hii imezifanya nchi nyingi za bara hilo zikabiliwe na tatizo la kushindwa kujidhaminia mahitaji muhimu kama chakula na dawa. Kuhusiana na hilo, Rais wa Senegal, ambaye ndiye Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, ametaka nchi maskini za bara hilo zipewe hadhi sawa na Ukraine na matatizo yao yashughulikiwe kwa heshima na hadhi ile ile inayopewa hivi sasa Ukraine.
Akizungumza katika mkutano wa nane wa Jukwaa la Kimataifa la Dakar, Rais wa Senegal, Macky Sall amesema: “Watu wa Afrika wanaamini kwamba, wakati huu ambapo Ukraine iko vitani na inashambuliwa, Afrika pia inashambuliwa na ugaidi; hata hivyo, hakushuhudiwi mshikamano wa kimataifa na Waafrika wanaosumbuliwa na mgogoro wa kiuchumi na aina ya tofauti za magonjwa.”
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika pia ametangaza kuwa kiwango cha uwakilishi wa bara hilo katika mashirika ya kimataifa, likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Kundi la 20, kinapaswa kuongezwa, na kwamba bara hilo linapaswa kuwa na mwakilishi.
Hapo awali, nchi nyingi za Kiafrika na za Kiislamu zilikosoa sera na misimamo ya kinafiki na kindumakuwili ya nchi za Magharibi kuhusiana na mzozo wa Ukraine. Nchi hizo zinaamini kuwa Wazungu waliofumbia macho vita katika nchi za Kiislamu zikiwemo Syria, Iraq, Afghanistan, Yemen na sehemu nyingine za dunia, sasa wanatoa wito wa kusaidiwa Ukraine dhidi ya Russia kwa kisingizio cha ukiukaji wa haki za binadamu, ingawa huko nyuma hawakuchukua hatua yoyote dhidi ya mashambulizi ya Marekani na waitifaki wake dhidi ya nchi tofauti za Kiislamu.
Kuanza vita vya Russia na Ukraine na kuendelea kwake, kumezifanya nchi nyingi za Kiafrika kukabiliwa na mazingira magumu na hivyo kuathirika vibaya na vita hivyo hasa katika suala zima za kujidhaminia chakula. Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, vita vya Ukraine vimesababisha kupanda kwa bei za vyakula na kufikia katika kiwango cha juu kabisa katika maeneo mbalimbali ya dunia. Filihali, kuna watu bilioni moja na milioni 700 duniani ambao ni sawa na theluthi moja ya wakazi wa dunia ambao wako chini ya mstari wa umasikini na wanataabika pakubwa kutokana na kukabiliwa na uhaba wa chakula.
Hii ni katika hali ambayo, mataifa ya Kiafrika hususan katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa yakikabiliwa na matatizo mbalimbali kama ongezeko kubwa la uhaba wa chakula, mabadiliko ya tabianchi, idadi kubwa ya watu na ukosefu wa vifaa muhimu vya afya na matibabu.
Hata hivyo kuanza vita vya Ukraine katika kipindi ambacho ulimwengu ulikuwa ukipitia kipindi cha baada ya janga la virusi vya Corona na taathra zake hasi ni jambo ambalo liliifanya hali ya nchi za Kiafrika kuwa mbaya zaidi.
Workneh Gebeyehu, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Serikali ya Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) anasema: Mshituko uliotokana na mabadiliko ya tabianchi, mapigano, uvamizi wa nzige na vita vya Ukraine ni mambo ambayo yameshadidisha njaa na ukosefu wa usalama wa chakula na hivyo kuwa kikwazo kwa juhudi za ustawi na maendeleo katika eneo.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya Russia na Ukraine kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa ilikubaliwa kutumwa mafurushi na mizigo ya nafaka mbolea za kemikali katika miezi ya hivi karibuni kwa nchi masikini za Kiafrika. Hata hivyo, sehemu kubwa ya mizigo hiyo imesafirishwa na kupelekwa nchi tajiri barani Ulaya kinyume kabisa na makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa.
Vasily Nebenzya, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa anasema: Kutopelekwa nafaka ya Ukraine kwa nchi zinazoendelea na zilizokumbwa na ukame barani Afrika ni jambo linalokinzana wazi na makubaliano ya hapo kabla.
Ukweli wa mambo ni kuwa, baada ya kuibuka vita vya Ukraine, madola ya Magharibi yamefumbia macho rasmi matatizo ya bara la Afrika na viongozi wa mataifa hayo wamekuwa wakitoa matamshi na misimamo ya kindumakuwili kuhusiana tu na matatizo ya Ukraine kama vile hakuna matatizo katika maeneo mengine duniani. Ni kutokana na ukweli huo, ndio maana Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika akakemea vikali ubaguzi, unafiki na undumakuwuili wa madola ya Magharibi na kutoa mwito wa nchi maskini za bara hilo kuzingatiwa na kupewa hadhi sawa na Ukraine na matatizo yao yashughulikiwe kwa heshima na hadhi ile ile inayopewa Ukraine na madola ya Magharibi.