Taliban yapiga marufuku masomo ya Chuo Kikuu kwa wanawake nchini Afghanistan

Serikali ya Taliban imesitisha elimu ya Chuo Kikuu kwa wanafunzi wote wa kike nchini Afghanistan, hatua ya hivi karibuni kabisa ambayo inakosolewa huku kundi hilo likituhumiwa kwamba, linakandamiza haki na uhuru wa wanawake wa nchi hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Elimu ya Juu ya Afghanistan ameithibitisha kusitishwa kwa elimu ya ngazi ya Chuo Kikuu kwa wanawake nchini Afghanistan. Taarifa ya Wizara hiyo imeeleza kuwa, uamuzi huo ulifikiwa  katika kikao cha baraza la mawaziri na kwamba, agizo hilo litaanza kutekelezwa mara moja.

Wasichana walizuiwa kurejea shule za upili mwezi Machi, baada ya Taliban kuamuru shule za wasichana kufungwa saa chache tu baada ya kufunguliwa kufuatia kufungwa kwa muda mrefu kwa miezi kadhaa baada ya kuchukua madaraka Taliban mnamo Agosti 2021.

Baada ya kuingia madarakani nchini Afghanistan, Taliban waliahidi kubadilika zaidi katika suala la kuheshimu haki za binadamu na haki za wanawake ikilinganishwa na kipindi walipokuwa madarakani mwaka 1996-2001.

Lakini wananchi wengi wa Afghanistan na jamii ya kimataifa wanaamini kuwa serikali ya kundi hilo imekuwa ikizibana hatua kwa hatua haki za Waafghani hasa wanawake, kwa kuwazuia kurudi maskulini na kutowaruhusu wanawake kufanya kazi katika sekta nyingi serikalini.

Kudhamini haki za msingi za wanawake, kufungua upya skuli zote za wasichana, kuhakikisha ardhi ya Afghanistan haitumiwi dhidi ya nchi zingine, na kuunda serikali pana na jumuishi ni miongoni mwa masharti yaliyotolewa na jamii ya kimataifa kwa ajili ya kuitambua serikali ya Taliban.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *