Tani 60,000 za makaa ya mawe kusafirishwa nje ya nchi

Songwe. Waziri wa Madini, Dk Dotto Biteko amesema Serikali inatarajia kusafirisha tani 60,000 za makaa ya mawe kupelekwa nje ya nchi baada wa Shirika la Madini Taifa (Stamico) kuanza uzalishaji katika mgodi wa Kiwira-Kabulo Wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe.

Dk Biteko amesema hayo leo Jumamosi Julai 2, 2022 alipofanya ziara kukagua miundombinu katika mgodi huo ambao unatarajia kuanza uzalishaji hivi karibuni.

Amesema kuwa tayari wameingia mkataba na Kampuni ya Aarthus Bearing SA (ABSA) ambayo itakuwa inasafirisha makaa ya mawe kwenye nje ya nchi kupitia Bandari ya Mtwara.

Waziri huyo amesema Serikali imeharakisha mchakato wa kufufua Shirika la Stamico ambalo lilisimama uzalishaji kwa kipindi cha miaka minne na hivyo kupoteza ajira kwa vijana na kuwepo kwa malimbikizo ya madeni kwa wafanyakazi.

”Wakati tunaharakisha kuanza mradi huu pia watumishi muwe na subra mtalipwa stahiki kwa wakati na mshirikiane na Serikali katika kuhakikisha mradi huu unapoanza unakuwa na tija kwa jamii na Serikali kwa ujumla ”amesema

Amesema Serikali imekusudia kuboresha na kutekeleza sera ya viwanda kwa kuwekeza na kufufua viwanda vilivyokufa ikiwapo mgodi wa makaa ya mawe Kiwira

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Stamico, Dk Venance Mwase amesema mikakati yao ni kuanza uzalishaji mkubwa ili kukidhi mahitaji ya masoko makubwa nje ya nchi kupitia Bandari ya Mtwara.

”Tayari tumesaini mkataba na kampuni itakayonunua tani 60,000 kwa mwezi huku na magari zaidi ya 300 yataingia kwa ajili ya kusafirisha shehena za makaa ya mawe.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Anna Gidalya amesema kuwa kusimama kwa mradi huo kumepunguza ajira kwa vijana na kupunguza mapato ya halmashauri.

”Tunashukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kufufua mradi huo ambao utanifaisha wananchi wa wilaya za Ileje na Kyela na Rungwe ambao ni majirani zetu”alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Stamico, John Angumbwike ameomba Serikali kuharakisha kuanza kwa mradi huo pamoja na kuwalipa stahiki zao.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *