Tanzania inaathirikaje Jerusalem ukiwa mji mkuu Israel

Huu ni uchambuzi uliotolewa na mchambuzi wa Gazeti Mwananchi kuhusu  kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem akisema:

Hivi karibuni Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel na kwamba ubalozi wake utahamishwa kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem.

Akitetea uamuzi huo, Trump alisema ulishapitishwa na Baraza la Congress miaka mingi, lakini ulikuwa hautekelezwi kwa sababu ya kusubiri usuluhishi wa mgogoro kati ya Israel na Palestina.

Uamuzi huo umezua tafrani kubwa duniani ikiwamo maandamano na vurugu zinazofanywa na Wapalestina.

Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga amenukuliwa hivi karibuni akipinga uamuzi huo na kusisitiza kuutambua mji mkuu wa Tel Aviv, lakini swali linabaki kuwa, Tanzania inaathirika nini ikiwa makao makuu yatahamishiwa Jerusalem?

Historia ya mgogoro kati ya Israel na Palestina ni wa muda mrefu tangu Taifa la Israel lilipoanzishwa mwaka 1945 kwa agizo la Umoja wa Matifa baada ya Waisraeli kunyanyaswa katika nchi walizokuwa uhamishoni.

Kuna nadharia nyingi za chanzo cha mgogoro huo, lakini iliyo kubwa ni historia ya Taifa la Israel inayoelezwa na kitabu cha Biblia ikionyesha kuwa eneo hilo la mgogoro liliahidiwa na Mungu kwa Waisraeli kupitia baba yao Ibrahim, lakini baadaye walikimbia kutokana na uvamizi wa mataifa ya kigeni ikiwemo Italia.

Tangu Taifa la Israel lilipoundwa tena mwaka 1945 baada ya vita ya pili ya dunia, limejikuta likijijengea maadui wengi ambao ni nchi za kiarabu zinazoizunguka, huku kwa upande mwingine ikiungwa mkono na Taifa kubwa la Marekani.

Kutokana na kuwa na maadui wengi, Israel imejiimarisha kijeshi kiasi cha kuonekana Taifa katili kwa Palestina kila unapotokea mzozo.

Moja kati ya matukio makubwa ya kujitetea kwa Israel ni vita ya siku sita iliyoanza Juni 5, 1967 ambayo Israel iliyashinda majeshi ya baadhi ya nchi za Kiarabu. Baada ya vita hiyo, Mwalimu Julius Nyerere akiwa Rais wa Tanzania alitangaza sera ya mambo ya nje akisema imeegemea katika uhuru na haki kwa wanadamu wote.

Tanzania haikuishia hapo kwani hata ubalozi wa Israel nchini ulifungwa na Mwalimu Nyerere aliendelea kushikilia msimamo wake hadi alipoondoka madarakani mwaka 1985.

Je, Watanzania tunapaswa kuendelea kufungwa na kongwa la kihistoria kwa mgogoro wa nchi nyingine au tufikirie upya?

Ukiifuatilia sera ya mambo ya nje aliyokuwanayo Mwalimu Nyerere wakati wake, utaona aliegemea katika uhuru na haki. Alijitolea rasilimali za Tanzania ili kuleta ukombozi kwa nchi nyingine hasa za Afrika.

Nathubutu kusema, miongoni mwa sababu zilizochangia kuirudisha nyuma Tanzania kiuchumi ni harakati za ukombozi wa mataifa mengine kama vile Msumbiji, Zimbabwe na alipinga ukandamizwaji uliokuwa ukifanywa na Israel kwa Wapalestina. Je, bado tunapaswa kuganda kwenye sera hizo? Dk Mahiga hana jipya zaidi ya kukumbatia historia?

Siungi mkono ukandamizwaji wa aina yoyote unaofanyika duniani, lakini tujue hakuna adui wa kudumu wala rafiki wa kudumu. Kinachodumu ni masilahi tu. Wema usizidi uwezo.

Kama ni kuunga mkono juhudi za ukombozi Tanzania imefanya vya kutosha, ifike mahali sasa masilahi ya kiuchumi yaangaliwe. Tanzania inafaidika nini, ikiwa leo Watanzania wanabaguliwa kwenye nchi ilizozitetea? Tanzania inafaidikaje kiuchumi kwa kuitetea Palestina? Tanzania inaathirika vipi kiuchumi Jerusalem ikiwa mji mkuu wa Israel?

Ifike mahali sasa Serikali ijikite kwenye diplomasia ya uchumi kuliko sera za kisiasa zisizo na masilahi mapana kwa wananchi. 0754 897 287

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *