Tanzania imepiga kura kuunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa linaloitaka Israel kukomesha uwepo wake wa “kinyume cha sheria” katika Ukanda wa Gaza.
Azimio hilo lililopitishwa, linaitaka Israel kujiondoa katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki ndani ya mwaka mmoja huku mzozo na Hamas ukikaribia kuadhimisha mwaka wake wa kwanza mnamo tarehe 7, mwezi Oktoba.
Azimio hilo ambalo ni la kwanza kuandikwa na Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) lilipitishwa kwa kuungwa mkono na nchi 124.
Uamuzi wa ICJ, ingawa haufungi, ulionyesha ukiukaji kadhaa, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa makazi na unyonyaji wa rasilimali.
Aidha azimio hilo linadai kuondolewa kwa majeshi ya Israel na kuondoka kwa walowezi kutoka katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
Inatoa wito wa kuwekewa vikwazo wale wanaodumisha uwepo wa Israel na kuhimiza kukomeshwa kwa uuzaji wa silaha kwa Israel iwapo zitatumika katika maeneo hayo.
Katika Afrika Mashariki, azimio hilo liliungwa mkono na nchi kadhaa miongoni mwao, Tanzania, Uganda, Djibouti, Burundi na Mauritius. Kenya, Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, na Sudan Kusini ni miongoni mwa nchi 43 zilizosusia azimio hilo.
Nchi 14 zikiwemo Israel na Marekani zilipiga kura dhidi yake.
Marekani ilikosoa azimio hilo, huku Balozi Linda Thomas-Greenfield akisema kuwa inashindwa kutambua Hamas kama shirika la kigaidi na inaweza kutatiza juhudi za kufikia suluhu ya mataifa mawili.
Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon, alilaani azimio hilo akisema ni la upendeleo na kupuuza jukumu la Hamas. Azimio hilo linampa kazi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kuripoti juu ya utekelezaji wake ndani ya miezi mitatu, ikiwa ni pamoja na hatua zilizochukuliwa na Israel, mataifa mengine na mashirika ya kimataifa.