Tanzania kuitumia Israel kutatua mgogoro wa Palestina

Haya yalikuwa ni maoni na mawazo ya mmoja wa Wanasiasa wa Tanzania kuhusu Palestina na Israel.

 

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Damas Ndumbaro amesema Tanzania haitaitenga Israel katika mchakato wa kusaka amani katika mgogoro wake na Palestina.

Hivi karibuni Balozi wa Palestina nchini Tanzania, Hamdi Mansour Abuali aliitahadharisha Tanzania kuhusu uhusiano wake na Taifa la Israel akisema imekuwa ikikiuka makubaliano na nchi yake.

Hata hivyo,  akizungumza katika maadhimisho ya siku ya Palestina jana usiku Jumatano Novemba 21, 2018 jijini Dar es Salaam, Dk Ndumbaro amesema Tanzania haitaitenga Israel kwa kuwa sera ya mambo ya nje ya nchi haifungamani na upande wowote.

“Ukiifahamu sera ya nje ya Tanzania ina misingi yake. Moja kati ya misingi ambayo Mwalimu (Julius Nyerere) alituachia ni kutofungamana na upande wowote. Maana yake ni kwamba unapochagua rafiki uchague kwa misingi inayofaa,” amesema Dk Ndumbaro aliyemwakilisha waziri wa wizara hiyo, Dk Augustine Mahiga katika sherehe hiyo.

“Tumekuwa na Wapalestina kwa muda mrefu lakini hivi karibuni umeona Israel nao wamekuja. La msingi hapa Tanzania tunaangalia kutafuta suluhu Mashariki ya Kati pasipo kubagua au kumtenga mtu yeyote.”

Amesema lengo la Tanzania ni kuziweka Palestina na Israel katika meza moja ya makubaliano ili wafikie mwafaka.

“Unapotafuta suluhu huwezi kuipata ukiwa na mtu mmoja, utaipata kwa ‘engagement’ au mtangamano. Ukiweza kuwaweka mezani Wapalestina na Israel wakaongea pamoja, suluhu itakuwa nzuri zaidi,” amesisitiza.

Amesema licha ya dunia nzima kutaka kuwepo kwa Taifa la Palestina lenye haki zake lakini haiwezekani kufumbia macho kuwepo kwa Taifa la Israel.

“Kuwe na kitu kinaitwa co-existence ambayo utaipata kama pande hizi mbili unaweza kuzileta pamoja mezani ziongee na zifikie mwafaka,” amesema.

Awali,  akihutubia katika sherehe hiyo, Dk Ndumbaro amesema Tanzania imekuwa na historia ndefu ya ushirikiano na Palestina lengo likiwa ni kupambana ili kuikomboa nchi hiyo.

“Sisi kama Tanzania ni wa kwanza kutambua uwepo wa chama cha kupigania uhuru cha Palestina yaani PLO na tulikuwa nchi ya kwanza kufungua ubalozi wa Palestina duniani, kwa hiyo tuna historia ndefu na Wapalestina,” amesema.

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Dk Ndumbaro, Abuali amesema lengo la sherehe hizo ni kuonyesha sanaa ya uchoraji inayoonyesha maisha halisi ya Wapalestina ili kuwapa faraja wananchi wa nchi hiyo wanaoteseka na vita dhidi ya Israel.

“Sanaa hii itasaidia kuibua na kuhalalisha hisia za wengi, hivyo kuleta faraja kwa machungu yaliyojificha. Itasaidia kuibua mambo kama mapambano ya Wapalestina na kuakisi mambo mabaya yanayowakuta ili kuwajengea ujasiri,” amesema Abuali.

Katika sherehe hiyo alikuwepo Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliyesisitiza msimamo wa chama hicho tawala nchini Tanzania kuwa ni kuwatetea wanyonge.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *