Wasomi nchini Tanzania wamesema kuuwa, wana matumaini ushirikiano kati ya taifa hilo na taifa la Romania utaongeza na kukuza uzalishaji katika sekta ya kilimo iwapo makubaliano yaliyotiwa Saini baina ya mataifa hayo yatatekelezwa kikamilifu.
Hayo yamelezwa kufuatia Marais wa mataifa hayo mawili, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mgeni wake Rais Klaus Iohannis kushuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano katika maeneo ya kimkakati ikiwemo sekta ya kilimo, mazingira na ushirikiano katika kukabiliana na majanga.
Mchambuzi wa mahusiano ya kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, Justine Kajerero anasema Tanzania ina nafasi ya kunufaika na makubaliano hayo iwapo makubaliano yatatekelezwa vizuri kwa vile makubaliano ya ushirikiano huo yameanzia katika taaluma, vyuo na wataalamu.
“Nafasi ya Tanzania kunufaika ipo iwapo makubaliano yatatekelezwa vizuri, na uzuri tofauti ya wao na wengine ukiangalia kilimo wananchokiongelea wameanzia katika mahusiano ambayo yatahusisha taaluma, vyuo, na wataalamu kwasababu wengi wamekuwa wakija mara nyingi wanakwenda moja kwa moja kwenye mazao tofauti na taaluma ambayo ndio itasaidia kukuza kilimo” amesema Kajerero.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, hati zilizosainiwa baina ya Tanzania na Romania zinahusu kukuza ushirikiano wa kiuchumi Kisayansi na Kiufundi katika sekta ya kilimo na mazingira pamoja na utiaji saini kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Romania kwa ajili ya kushirikiana katika kukabiliana na maafa na misaada ya kimataifa ya kibinadamu.
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa habari ameiomba Serikali ya Romania kuiunga mkono Tanzania katika mkutano wa Mabadiliko ya Tabia nchi wa COP28, 2023 utakaofanyika katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika ajenda yake ya nishati na nishati safi ya kupikia.
Rais wa Romania pia alikwenda Zanzibar ambako alikuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi Rais kabla ya hapo jana kuhitimisha ziara yake ya siku nne nchini Tanzania.