Tanzania imetangaza rasmi kupinga uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani kutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Akizungumza na gazeti la The Citizen, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk Augustino Mahiga amesema Tanzania kama ilivyo kwa jamii yote ya kimataifa haitambui Jerusalem au al Quds kuwa mji mkuu wa Israel. “Ubalozi wetu upo Tel Aviv na utaendelea kubaki hapo” amesema Mahiga na kuongeza kuwa, “kuna nchi zimetushawishi ila tutabaki Tel Aviv.” Waziri Mahiga hakutoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo. Kauli hiyo ya Mahiga imekuja baada ya vyombo vya habari vya Kizayuni kumnukuu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai akisema anaunga mkono tamko la Rais wa Marekani Donald Trump la kutambua al Quds kama mji mkuu wa Israel.
Akiwa safarini Israel, Ndugai alihojiwa na tovuti ya Kizayuni ya i24News na kusema anaunga mkono uamuzi wa Marekani kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Quds na kudai kuwa Tanzania nayo itafuata mkondo huo wa Marekani.
Katika hotuba yake ya jana Jumatano, Trump alidai kuwa, suala la kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni ilibidi lifanyike miaka mingi nyuma na kwamba serikali yake imechukua uamuzi huo ambao umewashinda marais wote waliotangulia wa Marekani. Uamuzi huo wa rais wa Marekani umelaaniwa kote duniani na hata waitifaki wake kama vile Ujerumani, Ufaransa na Uingereza pia wamepinga hatua hiyo ya Trump.