Hitilafu kubwa ya kiteknolojia iliyotokea asubuhi ya leo Ijumaa imesababisha mashirika makubwa ya ndege duniani kusitisha safari zao, mabenki kushindwa kutoa huduma kwa wateja, vyombo vya habari vya kimataifa kushindwa kurusha matangazo yao pamoja na kusimama kwa huduma nyingine nyingi zinazoendeshwa kwa kutumia teknolojia.
Hitilafu hiyo imesababishwa na matatizo ya kiufundi yaliyoikumba Kampuni ya Kimarekani ya Microsoft kupitia huduma yake ya Microsoft Cloud Computing, ambayo inatumiwa na karibu mashirika yote makubwa duniani kuendesha huduma na biashara zao.
Inaelezwa kuwa, hitilafu katika huduma hiyo ya Microsoft, imezilenga zaidi kompyuta zinazotumia mfumo wa uendeshaji wa Windows ambapo mamilioni ya kompyuta zinazotumia mfumo huo, zilijizima na kuonesha kiwambo au skrini ya rangi ya samawati.
Mashirika ya ndege kama American Airlines, Delta Airlines na United Airlines nchini Marekani, yote yametoa taarifa ya ndege zao zote kutua kwa dharura huku abiria wengi wakilazimika kusubiri kwenye viwanja vya ndege, wakiwa hawajui hatima yao.
Nchini Australia, uwanja mkubwa wa ndege wa kimataifa wa Sydney uliwatangazia abiria wote kwamba kutakuwa na kuchelewa kwa huduma za usafiri kutokana na tatizo hilo.
Barani Ulaya, Uwanja wa Ndege wa Brandenburg jijini Berlin, nao umetoa taarifa za kusitishwa kwa huduma zake zote huku nchini Uhispania, viwanja 46 vya ndege navyo vikisitisha huduma zake kutokana na tatizo hilo. Habari zaidi zinasema kuwa, treni za mwendokasi nchini Uingereza nazo zimeathiriwa na tatizo hilo na kusababisha huduma zote zisitishwe nchini humo.
Itakumbukwa kuwa, mwaka 2011, shirika la Microsoft lilidai kuwa, virusi vya kompyuta vilivyoathiri tarakilishi zinazotumia mfumo wa Windows wakati huo, vilitengenezwa na kusambazwa na shirika moja la utawala wa Kizayuni wa Israel.
Weledi wa masuala ya teknolojia wanasema kuwa, baadhi ya nyakati, taasisi za mawasiliano ya intaneti zinaeneza kwa makusudi virusi vya kompyuta ili ziweze kuuza bidhaa na programu zao za kukabiliana na virusi hivyo.