Times: Utumwa mamboleo bado upo nchini Saudi Arabia

Gazeti la Times la Uingereza limeripoti kuwa utumwa mamboleo ungalipo nchini Saudi Arabia licha ya maonyo ya taasisi za kimataifa.

Katika ripoti yake inayozungumzia uwepo wa utumwa mamboleo, kazi za kulazimishwa na ubakaji nchini Saudi Arabia, gazeti la Times limeandika kuwa, baadhi ya wafanyabiashara haramu ya binadamu nchini Saudi Arabia wanawaadhibu wafanyakazi wao kwa kuwapiga na wanawalipa wafanyakazi hao dola 6 tu mkabala wa kufanya kazi kwa takriban saa 24 kwa siku.

Ripoti ya gazeti la Times inasema, takriban wanaume na wanawake milioni nne wanaofanya kazi za nyumbani, kilimo au udereva nchini Saudi Arabia wamewekewa vikwazo vya aina mbalimbali, na waajiri wamewapokonya pasi zao za kusafiria.

Ripoti hiyo inasema: Nchini Saudi Arabia, wafanyakazi wa kigeni kwa namna fulani wako chini ya ufadhili na udhibiti wa waajiri wao, kwa kadiri kwamba raia wa Saudi ni sawa na wamiliki wa mfanyakazi huyo na ndio wanaoamua aina ya mkataba na masharti ya visa yake.

Mwaka jana, serikali ya Riyadh ilitangaza kwamba itarekebisha mfumo huo ndani ya mpango wa dira ya kimkakati ya 2030 ya Saudi Arabia na kwamba itadhamini haki za  wafanyikazi wa kigeni, ikiwa ni pamoja na kupewa ruhusa ya kufungua akaunti ya benki, kubadilisha kazi na uhuru wa kuondoka nchini humo. Hata hivyo kulingana na gazeti la Times la Uingereza, haki hizi hazidhaminiwa au kutekelezwa kwa wafanyakazi katika sekta ya kibinafsi, na makampuni ya gesi na mafuta.

Mwezi Septemba mwaka huu, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) liliripoti katika Umoja wa Mataifa kwamba mwaka 2021 watu wasiopugua milioni 50 duniani kote walikuwa wakiishi katika utumwa mamboleo, ambapo milioni 28 wanalazimishwa kufanya kazi za sulubu, na milioni 22 wako katika ndoa za kulazimishwa.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *