Ubelgiji: Kuzitumia mali za Russia zilizozuiwa kwa ajili ya kuijenga upya Ukraine si halali kisheria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji amesema si halali kisheria kutumia mali za Russia zilizozuiliwa, kwa ajili ya kuijenga upya Ukraine.

Nchi za Magharibi hasa Marekani zinajaribu kudhoofisha mfumo wa uchumi wa Russia kwa kushadidisha vikwazo, kuzuia na kupora mali za nchi hiyo kwa kisingizio cha vita vya Ukraine, ambavyo hadi sasa vimekuwa na matokeo kinyume na yaliyotarajiwa.
Kwa mujibu shirika la habari la IRNA Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji Hadja Lahbib amesisitiza kuwa kuzitumia mali za Russia zilizozuiwa katika nchi za Magharibi kwa ajili ya kuikarabati Ukraine hakuendani na utaratibu wa kisheria.
Hata hivyo Lahabib amedai kuwa utumiaji wa mali zilizozuiwa za Russia kwa ajili ya ujenzi mpya wa Ukraine ni wazo la kuvutia na akaongezea kwa kusema: Ubelgiji imezuia kiwango kikubwa cha mali za Russia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji amesema: Tunazo yuro bilioni 50 za mali za Russia zilizozuiliwa.

Kabla ya hapo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Ryabkov alisema kuzihamishia Ukraine mali za Russia au za raia wa Russia zilizozuiliwa ni sawa na wizi.
Umoja wa Ulaya na washirika wake katika Kundi la nchi saba tajiri wamezuia karibu yuro bilioni 300 (dola bilioni 311) akiba ya Benki Kuu ya Russia. Aidha, karibu yuro bilioni 19, mali za wafanyabiashara na wajasiriamali wa Russia waliowekewa vikwazo ziko mikononi mwa Umoja wa Ulaya.
Makadirio haya hayajakamilika na mali hizo ziko katika hali na mazingira yasiyojulikana na hivi sasa haziwezi kusambazwa wala kutumiwa.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *