Serikali ya kijeshi inayotawala Burkina Faso imeitaka Ufaransa iwaondoe wanajeshi wake katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi katika kipindi kifupi kijacho.
Chanzo cha habari ndani ya serikali hiyo kimenukuliwa na shirika la habari la Reuters kikisema kuwa, wanajeshi hao wa Ufaransa wametakiwa wawe wameondoka kikamilifu nchini Burkina Faso ndani ya mwezi mmoja ujao.
Haya yanajiri baada ya wananchi wa Burkina Faso kujitokeza mabarabarani katika mji mkuu Ouagadougou kushiriki maandamano dhidi ya Ufaransa, hatua inayoonesha jinsi ushawishi wa Paris katika nchi za bara la Afrika unavyoendelea kupungua.
Mamia ya waandamanaji hao wa Burkina Faso wanaituhumu Paris kuwa inaingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo na kuendeleza ukoloni mamboleo. Aidha waandamanaji hao huku wakipiga nara walisema Paris imeshindwa kutekeleza ahadi na majukumu yake katika mapambano dhidi ya makundi ya wanamgambo na ya kigaidi.
Moja ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao mjini Ouagadougou juzi Ijumaa lilikuwa limeandikwa “Ufaransa lazima iondoke.’
Burkina Faso ni koloni la zamani la Ufaransa, na kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo, Ibrahim Traoré amekuwa akieleza wazi hisia zake dhidi ya Wafaransa tangu aingie madarakani, na amepanua uhusiano na nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na Russia.
Mapema mwaka huu, serikali ya Burkina Faso ilimtimua balozi wa Ufaransa mjini Ouagadougou, Luc Hallade; hatua iliyochukuliwa katika kivumbi cha mvutano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.