Ufukara ndio uliosababisha vifo vingi vya baridi kali katika mji wa Buffalo, Marekani

Gazeti moja la Marekani limeandika kuwa, matatizo yaliyosababishwa na janga la kimbunga hatari na unyeshaji mkubwa wa theluji katika mji wa Buffalo yamedhihirisha zaidi ufukara na ukosefu wa usawa wa kiuchumi na wa mbari unaotawala katika mji huo wa Marekani kuliko ulivyowahi kushuhudiwa wakati mwingine wowote.

Mji wa Buffalo ulioko katika jimbo la New York, sambamba na kimbunga cha msimu wa baridi kali kilichoikumba Marekani, umeshuhudia pia mrundiko wa theluji na kimbunga kikali cha theluji kuwahi kushuhudiwa katika miongo minne iliyopita, pamoja na matukio ya uporaji na wizi.
Gazeti la Washington Post limeandika kuwa, katika mji wa Buffalo, masuala ya kimuundo kama vile umaskini, uhaba wa bidhaa za chakula, makazi duni na uwekezaji mdogo wa vitegauchumi vya serikali yamezidisha kiwango cha maafa ya kimbunga cha theluji katika maeneo ya wafanyakazi za vibarua, raia weusi na wale wa Kilatini.
Gazeti hilo limekosoa kukosekana usawa wa kijamii na kiuchumi katika mji wa Buffalo na kubainisha kuwa, masuala hayo yameufanya mji huo uonekane zaidi kuwa na mpasuko mkubwa wa kambi mbili za matabaka.
Gazeti la Washington Post limeeleza katika ripoti yake kwamba, watu wa Buffalo wameeleza manung’uniko yao ya kutoridhishwa na utendaji wa maafisa wa mji huo katika kukabiliana na maafa ya kimbunga na theluji na kubainisha kuwa, maeneo mengi ya vitongoji vyenye wakazi matajiri zaidi, wengi wao wakiwa ni wazungu yalikuwa yamejitayarisha vyema kukabiliana na kimbunga cha theluji. Aidha wamesema, mamlaka husika zilielekeza mipango na mikakati yao katika kukabiliana na athari za kimbunga katika maeneo hayo na kwamba hata gridi za umeme na mitandao ya barabara katika maeneo hayo ilikarabatiwa kwa haraka zaidi.
Buffalo, ambao ni moja ya miji maskini zaidi nchini Marekani,  ungali unakabiliwa na baa la ubaguzi wa rangi.
Hadi sasa watu 37 wameripotiwa kufariki dunia katika mji huo kutokana na athari za kimbunga cha baridi kali.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *