Uganda: Jeshi letu limemuua kiongozi wa waasi wa ADF katika shambulizi la hivi karibuni

Msemaji wa Jeshi la Uganda, Kanali Deo Akiiki ametangaza habari hiyo na kumtaja kiongozi huyo wa waasi kwa jina la Musa Kamusi. Hayo yamo kwenye taarifa ya jana Jumatano ya Kanali Akiiki.

Amesema: “Wanajeshi wetu waliokuwa wakiwawinda waasi wa ADF katika Hifadhi ya Kitaifa ya Kibale wamefanikiwa kumuua mmoja wa viongozi wa ADF ambaye amekuwa akiwahangaisha raia huko Kamwenge.”

Ameongeza kuwa, baada ya kumuua kiongozi huyo wa waasi wa ADF, jeshi la UPDF la Uganda limepata pia bunduki moja ya PK na bunduki moja ya AK-47 iliyokuwa na risasi kadhaa. Haya yameripotiwa siku moja baada ya waasi wa ADF kuwashambulia na kuua raia watatu wakiwemo watoto wawili huko Kamwenge.

Wiki iliyopita pia, waasi hao hao waliua watu 10 katika wilaya moja huko Uganda. Jeshi la nchi hiyo limeanza mchakato wa kuajiri askari wa vitengo vya ulinzi vya ndani ili kuimarisha usalama katika eneo hilo.

Kwenye sehemu moja ya taarifa yake, Kanali Akiiki amesema: “Vikosi vyetu vinaendelea kuwasaka waasi wa ADF walioua watu huko Kamwenge ili waangamizwe na ili raia waweze kuishi kwa usalama na amani.”

Mwezi uliopita, Jeshi la Uganda lilitangaza kuwa limeua waasi sita wa ADF na kumkamata kamanda anayeaminika kuhusika na mauaji ya watalii wawili wa kigeni na mwongozaji wao raia wa Uganda katika mbuga ya wanyama ya magharibi mwa nchi hiyo iliyoko karibu na mpaka wa DRC.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *