Viongozi kutoka takriban mataifa 120 duniani wamekusanyika katika mji mkuu wa Uganda, Kampala kwa ajili ya Mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) ulioanza jana Jumatatu.
Takriban wageni 4,000 kutoka mataifa mbalimbali wanachama walitarajiwa kuhudhuria mkutano wa kilele utakaoendelea kwa muda wa wiki moja unaolenga kushughulikia masuala muhimu ya kimataifa na kukuza ushirikiano kati ya nchi wanachama.
Wajumbe wa mkutano huo wameunda kamati mbili – za kisiasa, na za kiuchumi na kijamii – ambazo mazungumzo yao yataunda Hati ya Matokeo ya Kampala ambayo itapitishwa na mawaziri wa Mambo ya Nje na kuidhinishwa katika mkutano wa Wakuu wa Nchi Jumamosi ijayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Jenerali Jeje Odong, amesema dunia inahitaji ushirikiano wa pande nyingi na mshikamano ili kukabiliana na changamoto zake nyingi.
Katika kikao cha awali cha mkutano huo wa Kampala, Balozi wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Bw. Riyad Mnasour aliwataka wajumbe kujadili mgogoro kati ya Palestina na Israel, na kusema kuwa licha ya kuwa harakati hiyo inakumbana na changamoto nyingi, mgogoro huo wa Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) ni wa dharura zaidi.
NAM ilianzishwa mwaka 1961 katika kilele cha Vita Baridi kati ya Magharibi na Mashariki. Lakini, tofauti na mashirika mengine ya kikanda na kimataifa, haina mkataba rasmi wala sekretarieti ya kudumu. Nchi yenye uenyekiti wa mzunguko ina jukumu la kuratibu na kusimamia mambo ya Jumuiya.