Uganda yakosoa EU kwa kupinga Bomba la Mafuta la Uganda -Tanzania

Wabunge nchini Uganda wamekosoa azimio la Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) lililosema nchi hiyo na Tanzania zinapaswa kusitisha miradi ya maendeleo ya mafuta na gesi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Wabunge wa EU walipitisha azimio hilo Alhamisi, wakitaja hatari kubwa za mazingira na hali ya hewa zinazosababishwa na Uganda, Tanzania na kampuni ya mafuta ya Ufaransa, Total, katika kutengeneza Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Walisema kunapaswa kuwa na “mwisho wa shughuli za uchimbaji katika mifumo ikolojia inayolindwa na nyeti.”

Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki ndilo pambano la hivi punde zaidi kati ya Umoja wa Ulaya na Shirika la Total, ambalo EU imekuwa ikilishutumu kwa muda mrefu kwa kujikurubisha kwa Russia.

Baada ya kukamilika, bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania litakuwa bomba refu zaidi  linalopashwa moto duniani, lenye urefu wa kilomita 1,443 (maili 896).

Waziri wa Nchi wa Uganda anayehusika na Uhusiano wa Kimataifa, Henry Okello-Oryem, amesema wabunge wa EU wanapaswa kufanya kazi za kidiplomasia kwa kuzingatia msingi wa kuheshimiana.

Akizungumza na Shirika la Habari la Anadolu amesema, “Azimio hilo ni la kusikitisha kwa sababu wengi wa wale waliopiga kura ya ‘ndiyo’ hawana taarifa yoyote kuhusu Afrika. Kwa hivyo, hawataki Afrika iendeleze maliasili yake na bado ndiyo njia pekee ya kutatua baadhi ya matatizo yetu! Watu wetu wanaendelea kukata miti kama njia ya bei nafuu zaidi ya nishati, ikiwa hatutawapatia fursa kama vile gesi (LPG), nani atafanya hivyo?.”

Naibu Spika wa Bunge la Uganda Thomas Tayebwa amesema katika kikao kwamba azimio hilo linawakilisha ukoloni mamboleo na ubeberu wa hali ya juu dhidi ya Uganda na Tanzania.

Azimio hilo ni toleo lililohaririwa la mswada wa awali ambao ulikuwa umetaka kusitisha kabisa maendeleo ya mradi huo wenye thamani ya dola bilioni 3.8.

Balozi wa Uganda katika Umoja wa Ulaya, Ubelgiji, Uholanzi na Luxemburg, Mirjam Blaak, amesema azimio hilo “halijazingatia ukweli na limechochewa na vikundi vya watu wanaojitakia makuu.”

Wabunge wa Umoja wa Ulaya wamesema mradi huo utakuwa ni dharau kwa vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Lakini profesa wa mazingira wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala Katongole Hadija ameliambia Shirika la Anadolu kuwa azimio hilo ni sehemu ya ujanja wa nchi zilizoendelea kwa shabaha ya kuzuia nchi zinazoendelea kunufaika na maliasili zao.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *