Uganda yapasisha sheria ya kukabili mapenzi ya watu wa jinsia moja

Hatimaye Rais Yoweri Museveni ameupasisha kuwa sheria, Muswada wa 2023 wa kupiga marufuku nchini humo na kuwachukulia hatua kali wanaojihusisha na mahusiano ya kingono ya watu wa jinsia moja, licha ya maonyo na vitisho vya nchi za Magharibi.

Hayo yamethibitishwa leo Jumatatu na Spika wa Bunge la Uganda, Anita Among ambaye amesema kuwa, Rais Museveni amepasisha sheria hiyo kwa mujibu wa Sura ya 91(3)(a) ya Katiba ya Mwaka 2015.

Spika Among amesema, “Tumesimama kidete kulinda utamaduni, thamani na maazimio ya taifa letu, kwa mujibu wa malengo yetu ya taifa nambari 19 na 24, na pia kwa mujibu wa kanuni za sera zetu. Wananchi wa Uganda wamezungumza, na ni jukumu letu kuitelekeza sheria hii kwa uadilifu, kwa dhati na kwa njia madhubuti.”

Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu yeyote anayejihusisha na ngono za jinsia moja au “anayeshikilia” kuwa na vitendo hivyo anaweza kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka 10 jela.

Spika wa Bunge la Uganda amesisitiza kuwa, nchi hiyo ya Afrika Mashariki katu haitaunga mkono vitendo vichafu vya mapenzi ya watu wa jinsia moja na kueleza kuwa, lengo la sheria hiyo ni kuwalinda Waganda dhidi ya fitina ya mashoga na waungaji mko wao.

Machi mwaka huu, Bunge la Uganda lilipitisha muswada wa sheria hiyo inayoharamisha kujitambulisha kama mtu wa uhusiano wa jinsia moja au LGBTQ na kuzipa mamlaka madaraka makubwa katika kukabiliana na raia wa nchi hiyo wanaojihusiha na uovu huo.

Rais Yoweri Museveni amekuwa mstari wa mbele kulaani vikali mahusiano ya jinsia moja kwa muda mrefu, na mwaka 2013 alitia saini sheria ya kukabiliana na ufuska huo.

Wananchi waliowengi Uganda wanasema inahitajika kuwaadhibu wanaojishughulisha na harakati za kuhamasisha uhusiano wa jinsia moja, ambazo zinatishia maadili ya kitamaduni na kidini katika taifa hilo la Afrika Mashariki.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *