Ugiriki yaachilia huru meli ya mafuta ya Iran baada ya kukiuka amri ya Marekani

Serikali ya Ugiriki imebatilisha uamuzi wake wa hivi karibuni wa kuteka meli moja ya mafuta ya Iran na hivyo kukaidi mashinikizo ya Marekani ambayo ndiyo iliyoamuru meli hiyo ikamatwe.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jumanne ya Shirika la Bandari na Usafiri wa Baharini la Iran, serikali ya Ugiriki imeamuru meli hiyo iachiliwe pamoja na mzigo wake pamoja na kuwa Marekani ilikuwa inashinikiza iendelee kushikiliwa.

Taarifa hiyo imesema: “Serikali ya Ugiriki hatimaye imeamuru meli irejeshwe kwa mmiliki wake na hilo limewezekana kutokana na hatua madhubuti za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”

Ikumbukwe kuwa, wiki kadhaa zilizopita, Ugiriki ilisimamisha meli ya mafuta iliyokuwa inapeperusha bendera ya Iran.

Kufuatia hatua hiyo ya kichokozi, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC nalo liliamua kusimamisha meli mbili za mafuta za Ugiriki za Delta Poseidon na Pruden Warrior kutokana na kutofuata sheria za usafiri wa baharini wakati zilipokuwa zinavuka Ghuba ya Uajemi.

Hatua hiyo ya jeshi la IRGC la Iran ilichukuliwa baada ya Tehran kumwita balozi mdogo wa Ugiriki hapa Tehran na kumkabidhi malalamiko yake kufuatia kuzuiwa meli ya mafuta ya Iran huko Ugiriki.

Wiki iliyopita,  mahakama moja ya Ugiriki, Jumatano ilifuta hukumu ya awali iliyoiruhusu Marekani kuzuia meli ya mafuta ya Iran katika ufukwe ya Ugiriki.

Iran na Ugiriki zilikuwa na uhusiano mzuri kabla ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran na Ugiriki ilikuwa ikinunua kwa wingi mafuta ya Iran.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *