Haya ni baadhi ya maoni yaliotolewa na Watalaamu na Wachambuzi wa Siasa na uhusiano wa Kimataifa baada ya Tanzania kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel.
Mapema wiki hii historia ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Israel uliingia katika sura mpya. Dunia imeshuhudia Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Dk Augustine Mahiga akifungua ubalozi wa Tanzania jijini Tel Aviv.
Ufunguzi wa ofisi hiyo ulihudhuriwa na watu mbalimbali akiwamo Waziri wa Sheria wa Israel, Ayelet Shaked.
Kufuatia hatua hiyo Dk Mahiga ameitaja Israel kama nchi ya kuigwa kwa sababu licha ya changamoto za kimahusiano na baadhi ya jirani zake, imepiga hatua kubwa za maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo cha umwagiliaji, viwanda, matibabu na Tehama.
Kwa upande wa ulinzi na usalama, Waziri Mahiga anasema Watanzania hawataisahau Israel kwa kuwa ndiyo nchi iliyosaidia kuanzisha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Dk Mahiga akirejea kauli ya Rais John Magufuli ya hivi karibuni alipowapokea mawaziri wawili wa Israel kwa nyakati tofauti, amewakaribisha Waisrael kutembelea Tanzania kwa ajili ya utalii.
Anasema zaidi ya watalii 50,000 kutoka Israel hutembelea Tanzania kila mwaka lakini hawatoshi kutokana na wingi wa vivutio vilivyopo nchini.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Tel Aviv nchini Israel, Dk Mahiga anasema ufafanuzi kuhusu uhusiano huo utatolewa kwa kina wiki hii, hasa ili kufahamu ni mambo gani wamekubaliana.
Anasema shughuli hiyo imekwenda kwa mafanikio na zipo faida nyingi za kiuwekezaji ambazo zitapatikana.
Kwa upande wake, Waziri Shaked anabainisha kuwa Israel ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo kusaidia teknolojia ya kisasa kwenye kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji.
Hatua hiyo imegonganisha maoni ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia baina ya wanaosema Tanzania imetazama nyuma na kupingana na mtazamo wa enzi za Mwalimu Julius Nyerere kuhusu Israel na wanaoona tofauti.
Katika suala hilo, wengine wanasema kuchipua upya kwa uhusiano huo wanaona faida zaidi wakisema kutafungua fursa mpya za kiuchumi hususani katika masuala ya teknolojia ya kilimo na ulinzi kutokana na nchi hiyo kuendelea sana katika nyanja hizo.
Kupingana kwa kauli za wataalamu hao kunatokana na sababu za awali za Tanzania kutokuwa na uhusiano mzuri ikiwa ni pamoja na kutokuwa na balozi kati ya nchi hizo mbili, huku ikiwa na ubalozi Palestina ambao ni kwa mahasimu wa Israel.
Wanasema wakati wa Mwalimu Nyerere alikuwa anapinga ubaguzi wa rangi uliokuwa unaendelea nchini Afrika Kusini, Israel ilikuwa inawaunga mkono watu weupe waliokuwa wakiwabagua Waafrika weusi, jambo ambalo Tanzania isingekubalia nalo.
Tanzania ilikuwa mtetezi wa wanyonge na msimamizi wa demokrasia Afrika na duniani kote.
Akizungumzia suala hilo Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa (CFR), Dk Ahmed Mtengwa anaunga mkono hatua ya kufungua ubalozi kuwa itasaidia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
Pia, anasema uhusiano wa Tanzania na Israel hauwezi kuharibu uhusiano uliopo kati yetu na Palestina.
“Uhusiano wa Tanzania na Palestina hauzuii nchi kuanzisha ushirikiano na nchi nyingine, hatua hii inaweza kugeuka na kuwa sababu ya kutafuta suluhisho la kudumu katika mgogoro wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili – Israel na Palestina,” alisema katika mahojiano ya simu.
Maoni ya Mtengwa yanaungwa mkono na Mhadhiri mwenzake wa Chuo cha Diplomasia, Innocent Shoo anayesema kuwa uhusiano huo mpya utakuwa na fursa lukuki kwa Tanzania.
“Nchi itafaidika kupitia uhusiano huu mpya katika maeneo ya kilimo, usalama, dawa na kupata soko jipya kwa bidhaa za nchi.
Msomi huyo anaongeza; Tanzania itaendelea katika teknolojia ya kilimo kwa sababu Israel imeendelea katika sekta hiyo, na wakati huu ambapo tunataka kuwa na nchi ya viwanda uhusiano huu utatusaidia kufikia malengo,” anasema Shoo.
Anasema katika nchi za Mashariki ya Kati zinazofanya vizuri katika dawa Israel ni mojawapo, hivyo tutafaidika, lakini pia majeshi yao yana nguvu na ni ya kitaalamu, hivyo inaweza kusaidia kuboresha ya Tanzania pia.
Alifafanua kuwa uwepo wa jangwa katika nchi hiyo utasisimua soko jipya la kuuza mazao ya ngozi na nguo.
Hata hivyo, Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), Abdallah Kizauli anasema kuwakaribisha Waisrael nchini ni kuwasaliti Wapalestina na Mwalimu Nyerere.
Anasema siku zote Nyerere alikuwa na akili na kuwapigania wanyonge, hadi sasa Israel bado ina mgogoro wa siku nyingi na Palestina na sisi tumewatambua rasmi, bila shaka hilo halijakaa vizuri.
“Ingawa Tanzania inalenga katika mabadiliko ya kiuchumi, uwezekano wa kutafuta mataifa mengine ambayo yanaweza kutusaidia kufikia mabadiliko hayo tunao,” anasema Profesa Kizauli.
Hoja hizo zinachagizwa na ile inayotolewa na mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Mohamed Issa anayesema kuwa kufanya hivyo ni kuwa ndumilakuwili.
Anasema sababu zilizofanya Mwalimu Nyerere avunje uhusiano na Israel ni pamoja na udhalimu, dhuluma kutoka taifa moja kwenda jingine, jambo ambalo bado linaendelea kati ya nchi mbili za Israel inayoungwa mkono na Tanzania leo, na Palestina inayoendelea kukandamizwa.
Anasema hafahamu vigezo vipi vinatumika kufikia uamuzi huo kwa sababu vipo vitu vingi vinavyoonyesha kuwa uamuzi huo una ukakasi.
Anasema kama vimetumika vigezo vya kiuchumi, wapo sahihi japo ukakasi bado upo pale, kama wametumia vigezo vya kidiplomasia watakuwa wamefanya kitu tofauti na alichokuwa akikihubiri Mwaimu Nyerere aliyekuwa akipinga udhalimu.
“Kwa kutumia hoja za kiuchumi pekee na kuacha za kutetea wanyonge, kidiplomasia na haki za binadamu sidhani kama ni sawa, kwa sababu yapo mambo mengi ya kiuchumi yenye madhara lukuki, kwa mfano wawindaji haramu wananufaika kiuchumi, lakini wanalitia taifa hasara ndiyo maana wanapingwa kote duniani,” anasema
Issa anafafanua kuwa mgogoro wa Israel na Palestina haujapata ufumbuzi, kuwakaribisha na kufungua ubalozi nchini mwao ni kuenzi maneno na matakwa ya Mwalimu Nyerere kwa maneno huku vitendo vikienda kinyume naye.
“Kuna maneno kuwa mbona yapo mataifa ya Kiarabu yanayoungana na Wapalestina, ni kweli zipo nchi za Kiarabu zilizoungana nao, lakini suala letu ni tofauti kabisa. “Sisi hatukuvunja uhusiano wetu na Israel kwa sababu baadhi ya mataifa ya Kiarabu yalivunja au kuungana nao; tulifanya hivyo kupinga dhuluma na siku zote nchi yetu imejinasibu kuungana na nchi zinazokandamizwa, dhuluma tuliyokuwa tunaipinga bado inaendelea kule Israel,” anasema Issa.
Anafafanua kuwa hatua ya sasa si jambo jema kwa taifa kwa sababu inajulikana Mwalimu Nyerere alikuwa anapinga dhulma, lakini kinachotokea sasa ni kuziunga mkono kwa makusudi au kwa kuzifumbia macho.
“Tunasema tuliuwasha Mwenge ili kumulika hata nje ya mipaka yetu tulete tumaini, wanaopaswa kupewa tumaini ni kama tumewasaliti, kwa sababu bado wanakandamizwa na Waisrael.
Tanzania ilivunja uhusiano na Israel mwaka 1973 baada ya vita vya Yom Kippur. Inaelezwa kuwa Mwalimu Nyerere alifikia uamuzi huo kutokana na msimamo wa Tanzania katika kugombania nchi kujitawala na haki za Wapalestina kuwa na maamuzi ya kujiamulia mambo yao bila kuingiliwa na Waisrael.