Ujerumani, mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika joho la mtetezi wa haki za binadamu

Ujerumani, kama mwanachama wa Umoja wa Ulaya, pamoja na Marekani, imechukua mtazamo wa kiadui na kuingilia masuala ya ndani ya Iran wakati wa machafuko na ghasia za hivi karibuni.

Alhamisi iliyopita Ujerumani iliwasilisha ombi la kuitishwa kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa kisingizio kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulikiukaji haki za binadamu wakati wa machafuko ya hivi karibuni. Hata hivyo uchunguzi wa rekodi ya haki za binadamu ya Ujerumani unaonyesha historia mbaya kupita kiasi ya Berlin katika uwanja huu.

Katika kikao hicho nchi za Magharibi, ikiwemo Ujerumani, zilianzisha mashambulizi ya kipropaganda yaliyoratibiwa dhidi ya Iran na kutoa shutuma nyingi zisizo na msingi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock alidai kwamba: Tumeiomba Iran isimamishe ukandamizaji lakini jibu limekuwa ukandamizaji mkali zaidi. Akizungumzia machafuko ya hivi karibuni nchini Iran, Waziri Mkuu wa Ujerumani, Olaf Scholz, pia amesema kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba: “Lazima tuzingatie ukiukaji wa haki za binadamu (nchini Iran) na tuchukue hatua.”

Maafisa wakuu wa serikali ya Ujerumani kama Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo wametoa madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Iran na kujisahaulisha kwamba nchi hiyo iliupatia utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein, mada na zana za kutengeneza silaha za kemikali wakati wa vita na mashambulizi ya utawala huo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ambazo zilisababisha maafa makubwa katika nchi zote mbili za Iran na Iraq.

Suala hili linepewa mazingatio makubwa na maafisa wa serikali ya Iran. Katika vita hivyo vya kulazimishwa, Iraq ilifanya jumla ya mashambulizi ya kemikali 582, ikiwa ni pamoja na mashambulizi madogo, ya kati na makubwa sana ya majaribio ya silaha za kemikali. Kutokana na mashambulizi hayo, zaidi ya watu 10,000 waliuawa shahidi, takriban watu 100,000 walijeruhiwa na walihitaji matibabu endelevu, na watu 250,000 walipata majeraha madogo. Khadija Karimi, mwakilishi wa Iran katika kikao cha Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa amesema kuwa: “Ujerumani ndiyo iliyokuwa muuzaji mkubwa zaidi wa nyenzo na zana zilizohitajika kutengenezea silaha za kemikali kwa utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq wakati wa vita vyake dhidi ya Iran, na utumiaji mkubwa wa silaha hizo ulipelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa idadi kubwa ya Wairani.”

Nchi za Magharibi, hasa Ujerumani, zilikuwa na nafasi muhimu sana katika kutoa vifaa na mada za kemikali zilizohitajiwa na utawala wa Baath wa Iraq ili kuzalisha na kutumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya Iran, na suala hili ni miongoni mwa sababu za kimya na upuuzaji wa makusudi wa serikali za nchi za Magharibi na vyombo vyao vya habari kuhusu mashambulizi ya silaha za kemikali yaliyofanywa na Iraq dhidi ya Iran. Makumi ya makampuni ya kuzalisha kemikali yaliisaidia Iraq kuunda silaha za kemikali, mengi yakiwa ni ya Ujerumani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir Abdollahian ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: “Utawala wa Berlin, kama mdhamini mkuu wa silaha za kemikali za Saddam dhidi ya watu wa Iran, umefanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kwa miaka mingi kwa kuiwekea Iran vikwazo visivyo vya haki na vya kinyama. Sasa wanatumia kinafiki taasisi za “haki za binadamu” kwa ajili ya kukiuka zaidi haki za binadamu dhidi ya watu wetu, na yote haya kwa jina la eti kuonesha “mshikamano” wa uongo na Wairani.”

Takwimu zilizopo zinaonyesha ushiriki wa makampuni 85 ya Ujerumani, 19 ya Ufaransa, 18 ya Uingereza na makampuni 18 ya Marekani katika kuuzatiti utawala wa Saddam kwa silaha za kemikali. Ni vyema kutambua kuwa Ujerumani inajulikana kuwa nchi iliyotia saini Mkataba wa Geneva, na Umoja wa Ulaya unaruhusiwa kuzuia utengenezaji wa silaha za kemikali huko Ujerumani kwa kukagua viwanda vyake vya kemikali. Moja kati ya wauzaji wakubwa wa mada za kuzalisha mabomu ya kemikali huko Iraq ni kampuni ya Ujerumani ” Imhausen Chemie”, na vyombo vya habari vya Ulaya, hasa vya Ujerumani, vimechapisha nyaraka nyingi kuhusu suala hilo.

Ijapokuwa nchi mbalimbali zimeiuzia Iraq mada za silaha za kemikali, vifaa vya kiufundi na uhandisi na vichwa vya makombora na zilishiriki pakubwa katika utengenezaji wa silaha hizo hatari, lakini mchango na nafasi ya Ujerumani katika uwanja huu ilikuwa kubwa zaidi.

Vilevile hatupasi kusahau uhalifu na jinai kubwa zilizofanywa na wakoloni wa Kijerumani katika nchi mbalimbali duniani. Kama mfano tu, wakoloni wa Ujerumani waliua kwa umati makumi ya maelfu ya watu wa makabila ya Herero na Nama huko Namibia kwenye mauaji ya kuangamiza kizazi yaliyotokea baina ya mwaka 1904 na 1908 ambayo wanahistoria wanayataja kuwa ni mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20. Mauaji makubwa yaliyofanywa na Wajerumani na vilevile kitendo cha wakoloni hao cha kuwafukuza wanawake na watoto wadogo na kuwapeleka maeneo ya mbali majangwani kilisababisha vifo vya maelfu ya watu wa Namibia waliopoteza maisha kutokana na kiu na njaa. Wakoloni hao wa Kijerumani pia walijenga kambi za kuwatumikisha kwa nguvu raia wa Namibia.

Kwa utaratibu huo, Ujerumani inapaswa kukalishwa kwenye kiti cha mhalifu badala ya kujivika joho la kutetea haki za binadamu, na hatimaye ihukumiwe kwa matendo yake dhidi ya binadamu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *