Ujumbe wa UN wakutana na Ayatullah Sistani, unafuatilia jinai za Daesh

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa leo (Jumatatu) umekutana na kufanya mazungumzo na kiongozi mkuu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, Ayatullah Ali Sistani katika mji mtakatifu wa Najaf al Ashraf.

Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa unaoongozwa na Christian Ritscher, mshauri wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkurugenzi wa timu ya uchunguzi kuhusu uhalifu uliofanywa na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Iraq, umemtembelea Ayatullah Sayyid Ali Sistani nyumbani kwake huko Iraq.

Miongoni mwa malengo ya mazungumzo hayo ni kutoa taarifa kuhusu shughuli za ujumbe huo wa UN nchini Iraq na mafanikio yake katika kuwasaka na kuwahukumu magaidi wahalifu wa kundi la kiwahabi la Daesh.

Katika mazungumzo hayo Ayatullah Ali Sistani amepongeza ushindi mkubwa wa Wairaq dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh na kusisitiza kuwa, bila ya ushindi huo madhubuti, ingekuwa muhali kuweza kuwasaka na kuwaadhibu wanachama wa kundi hilo kutokana na uhalifu walioufanya dhidi ya Wairaq hususan jinai za mauaji, utekaji nyara, kushambulia, kubaka na kuwanajisi wanawake na kuharibu turathi za kale za Iraq.

Kiongozi huyo wa juu zaidi wa Waislamu nchini Iraq ametoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kuwahudumia watu walioathiriwa na vitendo vya kundi la kigaidi la Daesh hususan wakimbizi wa Iraq na amesisitiza ulazima wa kukombolewa wanawake wa Kiizadi na Waturkmeni wanaoendelea kushikiliwa na mabaki na wafuasi wa kundi hilo la kigaidi.

Kwa upande wake mkuu wa timu ya UN inayofuatilia uhalifu wa Daesh nchini Iran (UNITAD) ametilia mkazo udharura wa kuhukumiwa wanachama wote wa kundi hilo na kusema: Umoja wa Mataifa hauwezi kuwasahau watu wote waliopata mashaka na kuathiriwa na uhalifu wa ISIS.

Christian Ritscher amesema uhalifu wa kundi la ISIS ulitaka kuharibu utamaduni wa Iraqi na mfumo wa kijamii unaojumuisha pamoja watu wa mbari na dini tofauti wa Iraq.

Mnamo mwaka wa 2017, Iraq ilitangaza ushindi dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS baada ya mapambano makali ya miaka mitatu.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *