Gazeti la Times linalochapishwa Uingereza limefichua kuwa wanajeshi wa Ukraine walioshiriki katika uvamizi wa vikosi vya Kiev katika mkoa wa Kursk wa Russia, walipewa mafunzo na wataalamu wa kijeshi wa Uingereza katika kipindi cha wiki chache kabla ya kufanyika shambulio hilo la kushtukiza.
Mnamo Agosti 6, vikosi vya Ukraine vilianzisha shambulio kubwa zaidi dhidi ya ardhi ya Russia tangu ulipoanza mzozo wa kivita baina ya pande mbili Februari 2022. Kasi ya kuingia katika mkoa wa Kursk ilizimwa haraka na jeshi la Russia, lakini wanajeshi wa Kiev wangali wanashikilia vitongoji kadhaa vya mkoa huo.
Kwa mujibu wa Times, mwezi mmoja kabla ya kutumwa huko Kursk, baadhi ya askari wa Ukraine walipelekwa Uingereza ambako walishiriki kwenye mazoezi ya siku kadhaa pamoja na wanajeshi wa Uingereza, lengo kuu la kozi hiyo ya mafunzo likiwa ni kuelewa namna ya kuvamia majengo marefu.
Maafisa wa nchi za Magharibi wamefurahia na kuunga mkono uvamizi wa Ukraine katika mkoa wa Kursk wa Russia, lakini wamekanusha kuwa na taarifa zozote za awali kabla ya kufanywa operesheni hiyo au kuhusika nayo.
Hata hivyo, Mshauri wa Rais Vladimir Putin wa Russia na Katibu wa zamani wa Baraza la Usalama la nchi hiyo Nikolay Patrushev, wameliambia toleo la Ijumaa la gazeti la Izvestiakwamba uvamizi wa Kiev ulipangwa kwa ushiriki wa shirika la kijeshi la Magharibi NATO na kwa huduma maalumu zilizotolewa na nchi za Magharibi.
Hayo yanajiri huku Wizara ya Ulinzi ya Russia ikitangaza siku ya Ijumaa kuwa, tangu ulipoanza uvamizi huo, jeshi la Ukraine limepoteza wanajeshi wanaofika 2,860 na mamia kadhaa ya vifaa vya kijeshi, vikiwemo vifaru 41, APC 40, na mitambo mitatu ya kurushia maroketi aina ya HIMARS iliyopatiwa Kiev na Marekani…