Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza ambaye anatazamiwa kupanda ngazi na kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo amesema serikali yake haitasita kutumia silaha za maangamizi za nyuklia, iwapo nchi hiyo italazimika kufanya hivyo.
Liz Truss ambaye anaongoza katika mchuano wa kugombea kiti cha Waziri Mkuu wa Uingereza alisema hayo jana Jumanne mjini Birmingham katika mkutano wa wanachama wa chama tawala cha Conservative.
Akijibu swali aliloulizwa iwapo atakuwa tayari ‘kobonyeza kitufe’ na kuisafisha dunia ikilazimu, alisema, “Nadhani ni jukumu muhimu la Waziri Mkuu, na nipo tayari kufanya hivyo.”
Mwanasiasa huyo wa chama cha Kihafidhina hata hukutaja uwezekano wa yeye kutoa kipaumbele kwa suluhisho la kidiplomasia, ikabla ya kukhitari makabiliano ya nyuklia. Amesema yuko tayari kutumia silaha hizo hatari hata kama kutamaanisha kuusambaratisha ulimwengu kiukamilifu.
Haya yanajiri huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akionya kuhusu hatari ya kutokea vita vya nyuklia duniani. Alitoa onyo hilo Agosti Mosi mwaka huu wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kuangaliwa Upya Mkataba wa NPT wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia.
Mwezi Juni mwaka huu, Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) ilionya kuwa, akiba ya silaha hatari za nyuklia duniani inatazamiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka michache ijayo.
Mbali na Marekani na Russia, nchi nyingine tatu wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinazozimiliki silaha za nyuklia ni Ufaransa, China na Uingereza.