Katika hatua nyingine ya uingiliaji kati wa mambo, London imemuita nyumbani balozi wa Uingereza mjini Tehran eti kwa ajili ya mashauriano, kufuatia hatua ya Idara ya Mahakama ya Iran kumnyonga Ali Reza Akbari, aliyekuwa jasusi wa shirika la kijasusi la Uingereza la MI6.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak amedai kuwa, ‘Jibu letu kwa Iran haliishii kwa hatua ya leo (ya kumrejesha nyumbani balozi wake wa Tehran kwa muda usiojulikana). Tunatathmini hatua zaidi ya kuchukua (dhidi ya Iran).”
Mapema jana, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilimwita balozi huyo wa Uingereza mjini Tehran, Simon Shercliff, kutokana na uingiliaji wa London katika masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu.
Mwanadiplomasia huyo wa UK aliitwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ulaya Magharibi katika Wizara hiyo, ambapo Tehran ilimbainishia kuwa inalaani vikali uingiliaji wa Uingereza katika masuala ya ndani ya Iran, hususan masuala yanayofungamana na usalama wa taifa.
Balozi huyo aliitwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran hapo jana, siku ambayo Tehran ilitekeleza hukumu ya kumnyonga Ali Reza Akbari, aliyekuwa jasusi wa shirika la kijasusi la Uingereza la MI6.
Kitengo cha Habari cha Idara ya Mahakama ya Iran, jana Jumamosi kilitangaza kuwa, Akbari aliyekuwa na uraia pacha wa Iran na Uingereza amenyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ufisadi mkubwa katika ardhi na kuendesha vitendo vya kuhatarisha usalama wa ndani na nje ya Iran kupitia kulifanyia ujasusi shirika la kijasusi la Uingereza MI6.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak ameshindwa kuzuia na kuficha hamaki zake baada ya jasusi wa nchi hiyo kutiwa mbaroni na kunyongwa nchini Iran na amedai kuwa kunyongwa jasusi huyo ni kitendo cha kikatili na cha woga.
Wakati huohuo, Uingereza imetangaza kumuwekea vikwazo mwendesha mashtaka mkuu wa Iran, Mohammad Jafar Montazeri kutokana na kuhamakishwa na hatua ya Iran kumnyonga jasusi huyo wa MI6 ya UK.