Shirika la habari la SANA limeripoti kuwa mifumo ya ulinzi wa anga ya jeshi la Syria katika viunga vya Damascus imeanzishwa ili kukabiliana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni.
Vyombo vya habari vya ndani viliripoti Alhamisi asubuhi kwamba mlipuko ulisikika katika mji mkuu wa Syria, Damascus.Wakati huo huo baadhi ya duru zimeripoti kuwa, utawala wa Kizayuni umeishambulia Syria.
Shirika rasmi la Habari la Syria (SANA) lilitangaza kuwa mifumo ya ulinzi wa anga ya jeshi kwenye viunga vya Damascus imeanzishwa kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya utawala wa Kizayuni.
SANA ilisema milipuko hiyo ambayo inasikika ndani na karibu na Damascus, ilisababishwa na ulinzi wa anga kugongana na makombora ya maadui.
Dakika chache baadaye, shirika la habari la SANA lilinukuu vyanzo vya kijeshi vya Syria vikisema: “Mnamo saa 1:10 asubuhi mnamo Februari 24, 2022, adui wa Israel walirusha makombora kutoka kaskazini mwa Ziwa Tiberias, yakilenga maeneo karibu na mji wa Damascus. “Askari watatu waliuawa na uharibifu wa mali ulifanyika.”
Wiki iliyopita, utawala wa Kizayuni ulirusha kombora la moja kwa moja katika eneo la Qati lililopo karibu na mji wa Zakia, kusini mwa Damascus.
Serikali ya Syria imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa, utawala wa Kizayuni na waitifaki wake wa eneo na magharibi wanaunga mkono makundi ya kigaidi ya kitakfiri ambayo yanapambana dhidi ya serikali ya Syria.Jeshi la Syria limegundua mara kwa mara silaha na risasi zinazotengenezwa na Israel kutoka kwa makundi ya kigaidi yaliyoko nchini Syria.
Wapiganaji wa Kizayuni mara kwa mara hushambulia maeneo yenye lengo la mashariki na kaskazini magharibi mwa Syria, kwa kutumia anga ya Lebanon au kupitia Miinuko ya Golan inayokaliwa kimabavu.Vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vilivyoko nchini Lebanon vimeripoti mara kwa mara kwamba utawala wa Kizayuni kila siku unakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa na kukiuka anga ya Lebanon.