Umoja wa Afrika huenda ukachukulia jukumuu la kusimamia usalama katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakati huu juhudi za kikanda zikiendelea huku mikanganyiko ikishuhudiwa kuhusu maamuzi ambayo yamekuwa yakichukuliwa.
Mkataba wa Mfumo wa Addis Ababa, mchakato wa Nairobi, wa Luanda, utaratibu wa pamoja wa mkutano wa ukanda wa maziwa makuu, ni sehemu ya michakato mingi kuhusu hali ya usalama mashariki mwa DRC ambapo sasa inabidi kuongeza juhudi za nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kutuma vikosi vyake.
Wataalamu wanaona hii ni sawa viungo vikiwa vingi huharibu mchuzi, na inahitaji ufafanuzi zaidi kabla ya kuongeza wanajeshi wengine.
Haja ya kuwepo uratibu imedhihirika katika mkutano wa viongozi wa ukanda wa maziwa makuu jijini Bujumbura nchini Burundi Jumamosi iliyopita na Jumatatu katika mkutano wa Windhock nchini Namibia ambapo sasa wameamua kukutana tena chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika.
Mkutano wa pande tatu utayoyakutanisha mashirika yote ya kikanda, SADC, EAC na ICGLR lengo ikiwa ni kupanga uratibu wa michakato iliopo na kukubaliana juu ya vikosi mbalimbali vya kikanda hususan vile vya ukanda wa Afrika mashariki vilivyo huko tangu Oktoba mwaka 2022, ambavyo serikali ya Kinshasa imekosoa ufanisi wake na sasa ujio wa vikosi vya SADC ambavyo mamlaka yake itakuwa ni kushambulia.
Umoja wa Afrika umekubaliana na pendekezo la kufanyika mkutano huo ambao hata hivyo haukueleza ni wapi na lini utafanyika, licha ya kuthibitisha kuwa utafanyika kabla ya mwisho wa mwezi Mei kulingana na mjumbe wa umoja wa Afrika.