Umoja wa Afrika unafanya juhudi za kuitisha mkutano wa mapatano ya kitaifa nchini Libya

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika AU amesema kuwa umoja huo umekutana na vyama na mirengo tofauti ya Libya katika jitihada zake za kuitisha mkutano wa mapatano ya kitaifa nchini humo.

Akizungumza baada ya kufungwa mkutano wa kilele wa siku mbili wa AU nchini Ethiopia, Moussa Faki Mahamat amesema, kikao cha maandalizi ya mkutano huo wa maridhiano kilifanyika hivi karibuni katika mji mkuu wa Libya Tripoli.

Katika sehemu moja ya matamshi yake, Mahamat amesema: “Tumekutana na vyama tofauti na tunashirikiana navyo kuainisha tarehe na mahali pa mkutano wa kitaifa utakaofanyika chini ya uenyekiti wa kamati ya ngazi ya juu ya Umoja wa Afrika inayoongozwa na Rais Denis Sassou Nguesso wa Congo Brazzaville.”

Rais Nguesso, aliwasilisha ripoti yake kwa viongozi wa AU, ambao walipitisha wazo la kuandaa kongamano shirikishi la maridhiano ya kitaifa ya Libya na amesema, ana matumaini wa kufanikiwa mchakato huo wa amani.

Libya yenye utajiri wa mafuta imetumbukia katika machafuko tangu 2011 wakati mtawala wa muda mrefu Muammar Gaddafi alipong’olewa madarakani baada ya kukaa madarakani kwa miongo minne mfululizo.

Hali imekuwa mbaya zaidi tangu mwaka jana wakati bunge la Libya lilipoteua serikali mpya inayoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fathi Bashagha kuwa kiongozi wa serikali.

Lakini mkuu wa serikali iliyoundwa kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa na yenye makao yake mjini Tripoli, Abdul Hamid Dbeibeh, anasisitiza kuwa, hatokabidhi madaraka isipokuwa kwa mtu ambaye atachaguliwa na Bunge lililochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Libya. Mzozo huo umeleta hofu ya kurejea tena Libya kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *