Umoja wa Mataifa: kukithiri kwa mashambulio dhidi ya wakimbizi DRC ni jambo lenye kushtua

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) na washirika wake wameeleza kushtushwa na ripoti za mashambulizi nane makubwa yaliyotokea katika siku 10 za mwanzo wa mwezi huu wa Februari katika jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa mjini Geneva Uswisi inaeleza kuwa mashambulizi yaliyosababisha watu kuuawa, kutekwa nyara, uporoaji wa mifugo na chakula na kuchoma nyumba moto yamewaathiri zaidi wakimbizi wa ndani katika jimbo hilo la Ituri.

Boris Cheshirkov, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amesema kuwa, shirika hilo limetoa wito kwa pande zote zinazohusika kusitisha mara moja ghasia dhidi ya raia, wakiwemo waliokimbia makazi yao, ambao wengi wao wamelazimika kukimbia mara kadhaa.

Aidha amesema, wimbi la ghasia linafuatia shambulio baya kabisa lililofanyika tarehe mosi Februari katika eneo la Plaine Savo ambapo ni makazi ya wakimbizi wa ndani, pia katika eneo la Djugu, Ituri. Kadhalika katika tukio hilo, watu 62 waliuawa na wanamgambo wapiganaji huku wengine 47 wakijeruhiwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA, mwaka 2016 kulikuwa na wastani wa wakimbizi wa ndani milioni moja huku jumla ya wakimbizi wa ndani milioni 5.6 wakirekodiwa mwishoni mwa 2021.

UNHCR inazitaka pande zote kuruhusu mashirika ya kibinadamu kutoa msaada kwa wahitaji ili kuokoa maisha yao.

Shirika hilo limesisitiza kuwa vitendo vya utekaji nyara na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa misaada, ambayo pia yamekuwa yakiongezeka, lazima yakomeshwe ili raia waweze kuendelea na shughuli zao bila vitisho kwa usalama wao.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *