Umoja wa Mataifa umepuuza na kutupilia mbali takwa la serikali ya Taliban na hivyo kwa mara nyingine tena kukikabidhi kiti cha uwakilishi wa Afghanistan katika umoja huo kwa Nasir Ahmad Faiq Mwakilishi wa Kudumu wa Afghanistan katika Umoja wa Mataifa.
Katika hali ambayo serikali ya Taliban ilikuwa imemuarifisha Sohail Shaheen kwa ajili ya nafasi hiyo ili kuiwakilisha serikali hiyo na Afghanistan kwa ujumla katika Umoja wa Mataifa; umoja huo umekataa pendekezo hilo na kwa mara nyingine tena imembakisha Faiq kwa ajili ya kiti hicho. Serikali ya Taliban inataka Afghanistan iwe na mwakilishi wake katika Umoja wa Mataifa ambapo licha ya takwa la jamii ya kimataifa Taliban bado haijadhihirisha nia na hamu yake ya kuunda serikali shirikishi huko Afghanistan bali inasisitiza kuhodhi madaraka nchini humo.
Kwa msingi huo, Umoja wa Mataifa unaona kuwa Taliban haistahiki kuwa na kiti cha kuiwakilisha Afghanistan katika Umoja wa Mataifa kama serikali ya kitaifa na kamili.
Sayyid Issa Hosseini Mazari mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Afganistan anazungumzia hilo akisema: “Taliban haijatayarisha mazingira yoyote yanayohitajika kwa ajili ya mamlaka ya kitaifa huko Afghanistan. Hatua muhimu zaidi ni kuunda serikali jumuishi kwa kuyashirikisha makabila, makundi na mirengo yote ya kisiasa; makundi ambayo hata hivyo hayatambuliwi na Taliban.”
Afghanistan ni nchi iliyogawanyika katika makundi mbalimbali ya kikabila, kimadhehebu na kisiasa ambapo kila kikundi kinapigania kuwa na mgawo unaostahiki wa mamlaka na uongozi. Hata hivyo Taliban ambayo kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita ina uzoefu uliofeli katika kuiongoza Afghanistan inaendelea kupiga ngoma ya kung’angania madaraka na kusababisha wakuu wa makabila na viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo kukimbilia nje ya nchi. Kundi hilo aidha halichukui maamuzi yoyote kwa ajili ya kuendesha uchaguzi na kuishirikisha mirengo yote ya kisiasa na kikabila katika utawala wake, suala ambalo linaendelea kupingwa na kukosolewa na jamii ya kimataifa. Hivi karibuni pia Russia ililitaka kundi la Taliban kufanya juhudi za kuasisi serikali shirikishi ili kurejesha amani ya kudumu huko Afghanistan.
Ghulam Hussein Nasiri mchambuzi wa masuala ya kisiasa huko Afghanistan anasema:” Ili kutambuliwa kimataifa, Taliban inapasa kufuata na kukidhi vigezo vya serikali ya kitaifa na shirikishi; muhimu zaidi katika uga wa kisiasa ikiwa ni kuunda vyama na kuendesha chaguzi katika ngazi tofauti. Hii ni katika hali ambayo Taliban haiamini kivyovyote kutekeleza matakwa hayo na inaendelea kutilia mkazo kuhodhi pekee madaraka huko Afghanistan.”
Ala kulli haal, kutupiliwa mbali ombi la Taliban la kutaka Afghanistan iwe na kiti cha uwakilishi katika Umoja wa Mataifa kumedhihirisha kupingwa waziwazi aina ya utawala wa kundi hilo la wanamgambo huko Afghanistan; na hiyo inaonyesha namna Taliban ilivyoshindwa kuungwa mkono na mataifa mbalimbali ya dunia ili kutambuliwa kimataifa. Hii ina maana kwamba Taliban pamoja na kupita zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu utawala mpya wa Taliban ushike hatamu za uongozi; kundi hilo si tu limeshinwa kuwadhaminia haki zao wananchi wa Afghanistan khususan wanawake na mabinti wa nchi hiyo hata katika sekta ya elimu bali mirengo na makundi mengi ya kisiasa ya nchi hiyo imeachwa nje ya muundo wa utawala wa Taliban na kutawanyika kama wapinzani katika nchi mbalimbali.
Kwa msingi huo, hatua ya Umoja wa Mataifa ya kupinga Taliban kupewa kiti cha kuiwakilisha katika Umoja wa Mataifa inapasa kuchukuliwa kama tahadhari muhimu kwa kundi hilo; ambapo kama kundi hilo litaweza kubadili na kuangalia upya hatua na nyenendo zake basi litafanikiwa kuungwa mkono na jamii ya kimataifa na hivyo kujiandalia mazingira ya kutambuliwa kimataifa. Vinginevyo, Taliban haitakuwa na nafasi kimataifa. Hali ambayo pia inaibua changamoto kubwa kwa wananchi wa Afghanistan. Jambo hili linadhihirika kikamilifu katika ripoti za taasisi za kimataifa kuhusu kupungua misaada ya kimataifa kwa wananchi wa Afghanistan.