Umoja wa Mataifa : Tunahitajia kiasi cha dola milioni 205 kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa jimbo la Tigray

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, unahitajia kiasi cha dola milioni 205 kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa jimbo la Tigray.

Hayo yameelezwa na Stephane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa katika mkutano wake na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya umoja huo mjini New York na kueleza kwamba, asasi hiyo inahitajia kiasi cha dola milioni 205 kutoka kwa nchi wahisani ili uweze kuwahudumia raia milioni 1.6 ambao ni wakimbizi wa jimbo la Tigray.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amezitaka nchi wahisani kutekeleza ahadi zao ili kuhakikisha operesheni ya misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa jimbo la Tigray inafanyika kama ilivyopangwa.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza kuwa, takribani asilimia 40 ya wakazi wa jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Tathmini iliyofanywa na Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, watu milioni 4.6 ambao ni asilimia 83 kwenye jimbo la Tigray hawana uhakika wa kupata chakula na watu wapatao milioni mbili kati ya hao wamo katika hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na baa la njaa.

Japokuwa mivutano na vita baina ya jeshi la serikali kuu na waasi Tigray vimekuwepo kwa muda mrefu, lakini mapigano mapya yaliyozuka kuanzia Novemba mwaka juzi (2020) ni makubwa kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni. Mapigano hayo yalianza baada ya viongozi wa jimbo la Tigray kufanya mambo kinyume na matakwa ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kuhusiana na uchaguzi.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *