Umoja wa Mataifa unasaidia mamilioni ya waathirika wa mafuriko Pakistan

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba, yanawasaidia zaidi ya watu milioni 33 walioathirika na mafuriko nchini Pakistan baada ya mvua kunyesha kwa kiwango kikubwa na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1200.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umeeleza kusikitishwa na mafuriko ya Pakistan yaliyosababisha vifo zaidi ya 1200 na kati ya hivyo watoto ni takriban 400.

Taarifa ya shirika hilo imeeleza kwa masikitiko kuwa, miongoni mwa miundombinu iliyoharibiwa au kusambaratishwa kabisa na mafuriko hayo ni mamilioni ya nyumba, vituo vya afya na shule takribani 18,000 ambazo ima zimesombwa na maji au zimeharibiwa vibaya na mafuriko.

Watoto milioni 16 wameathirika na mafuriko haya, watoto milioni 3.4 wana uhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu na ufikishaji wa misaada umekuwa mgumu kuwafikia watoto hawa kwani madaraja zaidi ya 160 na zaidi ya kilometa 5000 za barabara zimeharibiwa.

Hata hivyo mwakilishi wa UNICEF nchini Pakistan Abdullah Fadil anasema juhudi za kuokoa maisha na kusambaza misaada ni za lazima, na UNICEF inasambaza vifaa vya kibinadamu katika majimbo yote yaliyoathirika.

Shirika jingine la Umoja wa Mataifa ni lile la kuhudumia wakimbizi UNHCR ambalo limetoa msaada wa haraka wa mahema, karatasi za plastiki, ndoo na vifaa vingine vya nyumbani katika mikoa iliyoathiriwa vibaya ya Khyber Pakhtunkwa na Balochistan, ambapo limesambaza mahema 10,000 na vifaa vingine vya msaada.

Kwa upande wake, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema lina wasiwasi mkubwa kwani tayari zimeanza kutolewa ripoti za wagonjwa wa kuharisha, matatizo ya ngozi, mifumo ya kupumua, malaria na ndengue.

Mwaka uliopita pia, mamia ya watu walifariki dunia na kujeruhiwa na nyumba nyingi zilibomoka kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kali za msimu zilizonyesha katika maeneo mbalimbali ya Pakistan.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *