Umoja wa Mataifa walaani kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu nchini Sweden

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu (kitabu kitakatifu cha Waislamu) nchini Sweden.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza msimamo huo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu nchini Sweden na akasema: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anaunga mkono kulaaniwa vikali hatua ya kukivunjia heshima kitabu kitakatifu cha Waislamu.
Jumamosi iliyopita, Rasmus Paludan, mkuu wa chama cha mrengo wa kulia chenye misimamo ya kufurutu mpaka cha Stram Kurs au kwa Kiingereza Hard Line cha nchini Denmark, aliichoma moto nakala ya Msahafu karibu na ubalozi wa Uturuki katika mji mkuu wa Sweden Stockholm huku kukiwa na ulinzi mkali wa polisi.

Kitendo hicho cha Paludan kimelaaniwa vikali na Waislamu duniani pamoja na nchi za Kiislamu, huku serikali ya Sweden ikikosolewa vikali kwa kutozuia kitendo hicho.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki, Misri, Kuwait, Muungano wa Falme za Kiarabu, Al-Azhar ya Misri, Baraza la Wanazuoni wa Kiislamu Duniani, Qatar, Saudi Arabia, Indonesia, Jordan, Morocco, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, Hizbullah ya Lebanon na Harakati za Hamas na Jihadul-Islami za Palestina ni miongoni mwa nchi na taasisi zilizochukua msimamo dhidi ya kitendo hicho cha kuchukiza, ambapo mbali na kukilaani vikali zimetaka kisirudiwe tena na kuwaadhibu wahusika wake.
Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *