Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu (OHCHR) imepongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kutangaza kuondoa marufuku kwa vyama vya siasa nchini humo kufanya mikutano ya hadhara.
Msemaji wa ofisi hiyo kutoka Nairobi, Kenya Seif Magango amesema kuwa, “hatua hii ambayo ameichukua Rais Samia Suluhu Hassan ya kutupilia mbali marufuku dhidi ya mikutano ya vyama vya siasa nchini Tanzania ni nzuri na pia ushindi mkubwa kwa demokrasia na haki za binadamu, ikiwemo haki ya watu kukusanyika kwa amani na pia kujieleza kama wanavyotaka.”
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania Jumanne iliyopita alikutana na viongozi wa vyama 19 venye usajili kamili wa siasa nchini humo ambapo sambamba na kutangaza kuondoa marufuku hiyo alisisitiza kuwa, ni haki kwa vyama vya siasa kuendesha mikutano yao ya hadhara nchini humo lakini kuna wajibu wa kila mmoja na upande wa Serikali kuhakikisha mikutano hiyo inafanyika salama.
Mikutano ya hadhara ya kisiasa ilipigwa marufuku nchini Tanzania wakati wa urais wa Dk John Pombe Magufuli, hatua ambayo ililalamikiwa sana ndani na nje ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Tangazo la Rais Samia la kuondoa marufuku ya mikutano ya hadhara ya kkisiasa limepokewa kwa hisia tofauti ambapo baadhui wamepongeza hatua hiyo huku wengine wakisema, hakuna kikubwa kilichofanyika kwani hiyo ni haki ya kikatiba. Wapinzani nchini Tanzania kwa upancde wao wanasema kuwa, wapinzani wamepokea kwa tahadhari hatua hiyo. Kundi jingine la wapinzani nchini Tanzania linasema, hiyo ni fursa waliokuwa wamepokonywa na kwamba, sasa wataitumia kuikosoa serikali.