Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Korosi amepongeza agizo la Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei la kutoa msamaha kwa idadi kubwa ya wafungwa wa Iran na kusema kuwa hatua hiyo inastahili kupongezwa.
Korosi aliyasema hayo Jumanne alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian kando ya kikao cha 52 cha kawaida cha Baraza la Haki za Binadamu katika mji wa Geneva Uswisi.
Tarehe 5 Februari, Ayatullah Khamenei alisamehe au kupunguza hukumu za idadi kubwa ya wafungwa waliokamatwa wakati wa ghasia za hivi karibuni nchini Iran zilizoungwa mkono na madola ya kigeni,
Ayatullah Khamenei alitoa msamaha huo kwa mnasaba wa kutimia miaka 44 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yalihitimisha utawala wa Pahlavi ulioungwa mkono na Marekani hapa nchini mwaka 1979. Aidha alitoa msamaha huo kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Ali (AS). Kiongozi Muadhamu hutoa msamaha kama huo mara kwa mara wakati wa sherehe za kidini.
Korosi pia ameishukuru Iran kwa kuwapa hifadhi zaidi ya wakimbizi milioni tano wa Afghanistan licha ya changamoto zinazoikabili kutokana na vikwazo vya nchi za Magharibi.Vile vile ameeleza matumaini ya kurejea mazungumzo kati ya pande zinazohusika katika mapatano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015, yanayojulikana kwa jina la Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ili kufufua makubaliano hayo ambayo amesema yatakuwa kwa manufaa ya amani na usalama wa dunia.
Korosi pia ameshukuru uwepo wa Iran katika mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva.
Amir-Abdollahian kwa upande wake amesisitiza kuwa, kuheshimiwa haki za binadamu kunatokana na utamaduni na imani ya Iran na kutoa hakikisho kwamba Jamhuri ya Kiislamu itaendeleza ushirikiano wake na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa.
Amir-Abdollahian aliwasili Geneva Jumatatu asubuhi kwa ajili ya kuhudhuria na kuzungumza katika mkutano wa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa.