Umoja wa Mataifa umetangaza kupunguza misaada yake ya chakula kwa nchi ya Somalia katika kipindi hiki ambacho nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inakabiiliwa na hali mbaya ya ukame na uhaba wa chakula.
Ripoti zinasema, Umoja wa Mataifa umechukua hatua hiyo katika hali ambayo, Somalia inakabiliwa na hali ya njaa kali ambapo theluthi moja ya watu nchini humo wakitarajiwa kukabiliwa na mzozo au viwango vibaya zaidi vya mahitaji ya chakula.
Kwa mujibu wa gazeti la Russia Today, Mkuu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, Cindy McCain, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, takwimu za hivi punde za usalama wa chakula zinaonyesha kuwa, zaidi ya Wasomali milioni 6.6 wanahitaji msaada wa dharura wa chakula.
Utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya ya Uswisi, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) unaonyesha kuwa, ukame ambao ni mrefu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Somalia umesababisha makumi ya maelfu ya watu kupoteza maisha.
Matokeo ya utafiti huo yanasema kuwa, zaidi ya watu 43,000 yumkini waliaga dunia kutokana na janga la ukame lililoikumba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika mwaka 2022.
Hivi karibuni, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia alitahadharisha kuwa, vifo zaidi vitarekodiwa nchini humo na vitapindukia idadi ya watu waliopoteza maisha wakati njaa ilipoiathiri nchi hiyo mwaka 2011; ambapo watu zaidi ya 260,000 waliaga dunia kwa kukosa chakula.