Umoja wa Mataifa washtushwa na mauaji ya watu 50 nchini Mali

Mkuu wa Ofisi ya Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kusikitishwa na mauaji ya karibuni ya makumi ya watu nchini Mali.

Katika taarifa jana Alkhamisi, Volker Turk amesema ameshtushwa na mauaji ya kiholela yaliofanywa na jeshi la Mali na askari ajinabi dhidi ya raia 25 katika kijiji cha Welingara katika eneo la Nara, katikati ya Mali mnamo Januari 26.

Aidha afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa amesema ametamaushwa na ripoti za kuuawa watu 30 katika mashambulizi yaliyofanywa na magenge yasiyojulikana na wabeba silaha katika vijiji vya Ogota na Oimbe eneo la Bandiagara katikati mwa nchi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya utawala wa kijeshi nchini Mali kutangaza kusitisha makubaliano muhimu ya amani ya mwaka 2015 yaliyotiwa saini na makundi ya Kaskazini yanayotaka kujitenga, kufuatia miezi kadhaa ya uhasama kati ya waasi hao na jeshi.

Serikali ya mpito ya kijeshi iliingia madarakani nchini Mali mnamo Mei 2021 kupitia mapinduzi ya kijeshi. Disemba mwaka jana, Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Mali (MINUSMA) kilitangaza kuhitimisha rasmi majukumu yake nchini humo baada ya kuhudumu kwa muda wa miaka kumi.

Kuondoka kwa kikosi cha MINUSMA ni sehemu ya kurekebisha upya  mpango wa  usalama ulioanzishwa na utawala wa kijeshi wa Mali uliochukua mamlaka mwaka 2020.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *