Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka viongozi wa Lebanon kufanya kazi kwa pamoja ili kutatua migogoro iliyopo nchini humo, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuisaidia na kuiunga mkono Lebanon kutokana na matatizo yake ya sasa.
Faraan: Antonio Guterres ametoa wito huo wakati wa mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari uliofanyika katika Ikulu ya Rais nchini Lebanon na Rais wa Lebanon Michel Aoun.
Katika mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewaambiwa waandishi wa habari kwamba, “Nimekuja Lebanon na ujumbe mmoja rahisi, Umoja wa Mataifa unasimama kwa mshikamano na watu wa Lebanon.”
Ziara hiyo inalenga kujadili njia bora za kuwasaidia watu wa nchi hiyo kuondokana na mgogoro wa sasa wa kiuchumi na kifedha na kukuza amani, utulivu na maendeleo endelevu.
Katika hotuba yake ya kumkaribisha, Rais Aoun alisema kuwa mkutano wao umegusia suala la wahamiaji wa Syria na kwamba amemwambia Katibu Mkuu wa UN kuwa “Kuna haja ya kutafuta mbinu mpya ya suala la Wasyria waliokimbilia nchini Lebanon,” akibainisha kuwa mgogoro huu umekuwa ukiendelea na kuongezeka kwa zaidi ya miaka 10, na umekuwa mzigo mkubwa kwa Lebanon hasa katika hali inayolikabili taifa hilo hivi sasa.
Rais wa Lebanon alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua majukumu yake na kuhimiza kuwarejesha salama wakimbizi hao katika vijiji na nchi yao.