Umoja wa Mataifa wazindua muongo wa lugha za asili

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limezindua Muongo wa Lugha za Jamii ya Asili, katika kikao kilichoitishwa na Rais wa Baraza hilo, Csaba Kőrösi.

Akifungua mkutano huo, Kőrösi amesema lugha ni msingi muhimu katika ufahamu hali kadhalika katika utambulisho wa kila jamii.

Hata hivyo amesema kadri lugha za jamii ya asili zinavyotoweka,  ndivyo unavyotoweka utamaduni, mila na ufahamu ambao lugha hizo zimebeba.

Ametoa wito kwa nchi wanachama kushirikiana na jamii za watu wa asili ili kuchukua hatua kuu tatu.

Hatua hizo ni mosi; kulinda haki za watu wa jamii ya asili, kama vile elimu kupitia lugha zao mama. Pili; kuhakikisha watu wa jamii ya asili na ufahamu walio nao wa kiasili havitumiki vibaya na wapatiwe taarifa ya awali pindi watu wanapotaka kutumia ufahamu au lugha zao. Tatu; kushauriana na watu wa jamii ya asili, kuwashirikisha katika kila mchakato wa maamuzi yanayowahusu.

Muongo wa Lugha za jamii ya asili duniani 2022 hadi 2032 unalenga pia kuhamasisha juu ya kasi kubwa ya kutoweka kwa lugha za asili na hivyo hatua za haraka zichukuliwe kulinda ili kuziendeleza kitaifa na kimataifa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na  Utamaduni, UNESCO kwa kushirikiana na Idara ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi na Kijamii, UNDESA Pamoja na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za binadamu, OHCHR, zimeanzisha kikosi kazi cha kimataifa cha kuchukua hatua wakati wa muongo huu na hatimaye kuhakikisha kila mdau anashiriki.

Miongoni mwa lugha za asili ambazo zinaelezwa kuhifadhiwa kizazi na kizazi ni lugha ya Kimasai inayozungumzwa na jamii hiyo iliyo Tanzania na Kenya.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *