Umoja wa Ulaya washindwa kulaani uchochezi wa waziri mwenye itikadi za kibaguzi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa al-Aqsa.

Kitendo cha uchochezi cha waziri mwenye itikadi kali na za kibaguzi wa baraza la mawaziri la utawala haramu wa Israel katika kuuvunjia heshima Msikiti wa al-Aqsa hakijakabiliwa na hatua yoyote ya maana kutoka kwa Umoja wa Ulaya.

Itamar Ben-Gvir, waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni aliingia katika Msikiti wa al-Aqsa Jumanne iliyopita akifuatana na polisi wa utawala huo ghasibu, akiwa ni waziri wa kwanza wa baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu kuuvunjia heshima msikiti huo mtukufu wa Waislamu, baada ya miaka mitano.

Kitendo hicho cha Itamar Ben-Gvir kimekabiliwa na hisia na upinzani mkali kutoka kwa nchi nyingi duniani.

Nasser Kan’ani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amelaani vikali kitendo hicho cha kuvunjiwa heshima Msikiti wa al-Aqsa na waziri huyo wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wapalestina wametangaza kuwa, kuingia mawaziri wa utawala wa Kizayuni katika Msikiti wa al-Aqsa kunamaanisha kukiukwa hadhi ya kisheria ya maeneo matakatifu katika ardhi za Palestina.

Kupitia maneno laini na yasiyo na umuhimu wowote, kufuatia kuvunjiwa heshima Msikiti wa al-Aqsa na waziri huyo wa Kizayuni, Peter Stano, Msemaji wa Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, jana Jumatano, aliwataka Mawaziri wa utawala huo haramu na wa kibaguzi kupunguza mivutano na kudumisha hali ya sasa ya maeneo matakatifu huko Beitul Muqaddas.

Msikiti wa al-Aqsa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Palestina huko Beitul Muqaddas na utawala wa Kizayuni unajaribu kuharibu utambulisho huo, lakini kusimama na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kuufanya ushindwe kufikia malengo yake haramu katika ardhi za Wapalestina.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *