UN: 2022, mwaka wa mauaji zaidi katika ardhi za Palestina katika miaka 16 iliyopita

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika Maeneo Yanayokaliwa kwa Mabavu ametangaza katika ripoti yake kwamba mwaka huu wa 2022 ulikuwa mwaka wa umwagaji damu zaidi katika ardhi za Palestina katika kipindi cha miaka 16 iliyopita.

Ili kufikia malengo yao ya kujipanua zaidi, Wazayuni wamekuwa wakishambulia maeneo tofauti ya Palestina na kuuawa shahidi, kuwajeruhi au kuwatia nguvuni raia wasio na hatia. Mashambulizi ya Wazayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina hususan watoto wa Kipalestina, yameongezeka Katika wiki za hivi karibuni.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ma’an la Palestina, Lucia Elmi, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika Maeneo Yanayokaliwa kwa Mabavu amesema mwaka huu wa 2022, Wapalestina wasiopungua 105 wakiwemo watoto 26 wameuawa shahidi na majeshi ya Israel, hivyo mwaka 2022 umekuwa mwaka wa umwagaji damu zaidi tangu 2006.

Elmi ameongeza kuwa wastani wa wahanga wa Kipalestina kwa mwezi umeongezeka kwa asilimia 57 ikilinganishwa na mwaka jana.

Amesema kuwa idadi ya Wazayuni walioangamizwa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan mwaka 2022 ni 17.

Elmi ameeleza kuwa tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Oktoba, Wapalestina 15 wakiwemo watoto 6 wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds tukufu.

Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika Maeneo Yanayokaliwa kwa Mabavu ameashiria vikwazo vilivyowekwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu kusafiri katika maeneo ya Shuafat, Quds Mashariki na Nablus na kusema kuwa, hatua hizo zimepunguza uwezo wa watu wengi kupata huduma za elimu, afya na riziki.

Elmi ameeleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la vitendo vya ukatili na vikwazo vilivyowekwa na Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordani, ikiwa ni pamoja na Quds Mashariki.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *