Mashirika sita ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa masuala ya kibinadamu wametoa tahadhari ya baa la njaa kunyemelea eneo la Afrika Mashariki baada ya miaka minne ya ukame mkali huku ikitabiriwa uhaba wa mvua kwa mwaka mwingine wa tano mfululizo.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa mjini Nairobi Kenya na mashirika ya Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, la chakula na kilimo FAO, la kuhudumia watoto UNICEF, la kuhudumia wakimbizi UNHCR, la utabiri wa hali ya hewa WMO na la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA pamoja na washirika wengine wa masuala kibinadamu imesema, Somalia na maeneo kadhaa ya Kenya na Ethiopia yameathiriwa na baa la hali mbaya ya ukame ambayo haijawahi kushuhudiwa kwa miaka 40 sasa, ambapo misimu minne mfululizo ya mvua imekuwa na kiwango cha chini sana cha mvua.
Taarifa hiyo ya pamoja imesema, zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makazi yao Somalia na kusini mwa Ethiopia.
Upungufu wa maji uliopo umechochewa na hali mbaya ya joto la juu sana ambalo linatabiriwa kuendelea hadi msimu wa kiangazi wa Juni-Septemba.
Hali katika maeneo ya malisho inatarajiwa kuwa itazorota haraka kuliko kawaida na kusababisha vifo vingi vya mifugo, na pia kuhama kwa idadi kubwa ya watu.
Taarifa hiyo imeendelea kusema, katika maeneo ya kilimo, mavuno yatakuwa chini ya wastani, na hivyo kusababisha utegemezi mkubwa wa watu kununua chakula sokoni kwa muda mrefu, ambapo kaya nyingi zitashindwa kukidhi mahitaji ya chakula kutokana na bei ya juu ya chakula.
Ethiopia, Somalia na Kenya pia zimerekodi idadi kubwa zaidi ya watoto wenye utapiamlo waliolazwa kwa matibabu katika robo ya kwanza ya mwaka 2022 ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Taarifa hiyo ya UN imesisitiza kuwa, hatua za haraka zinahitajika sasa ili kuokoa maisha na kuepusha baa la njaa na vifo.