Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesema leo Ijumaa kwamba “ameshtushwa” na ongezeko la ghasia karibu na mji wa El Fasher huko magharibi mwa Sudan.
Volker Türk ameleza hayo huku Umoja wa Mataifa ukionya kwamba, umepokea asilimia 12 tu ya ufadhili unaohitajika kukabiliana na mgogoro wa binadamu nchini Sudan.
Türk amesema kuwa, wiki hii amefanya majadiliano na viongozi kutoka pande zote mbili za mzozo, akionya juu ya janga la binadamu iwapo mji huo utashambuliwa.
Amesema, amewaonya makamanda wa pande mbili kwamba mapigano katika mji wa El Fasher yatasababisha maafa na kuzidisha hali mbaya.
Jana, Alhamisi, Sudan ilipinga tamko la Umoja wa Ulaya kuhusu hali ilivyo katika mji wa El Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini, na shutuma zilizotolewa dhidi ya jeshi la nchi hiyo kuwa linafanya mashambulizi ya kiholela, sawa kabisa na Vikosi vya Msaada wa Haraka, RSF.
Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Ulaya ililaani mapigano makali yanayotokea El Fasher kati ya jeshi la serikali na Vikosi vya Msaada wa Haraka, ambayo yamesababisha hali mbaya kwa raia, na kutoa wito kwa pande zinazohusika katika mzozo wa Sudan kuruhusu mara moja na bila kizuizi kupelekwa misaada ya kibinadamu huko El Fasher.
Jumuiya za kimataifa zimesidisha miito ya kuiepusha Sudan na janga la binadamu ambalo linaweza kuwatumbukiza mamilioni ya watu katika njaa na vifo, kutokana na uhaba wa chakula unaosababishwa na mapigano ambayo yameenea katika majimbo 12 kati ya 18 ya nchi hiyo.