UN: Thuluthi moja ya Waarabu wanaishi katika umaskini

Taasisi ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, thuluthi moja ya jamii ya Waarabu wanaishi katika hali ya umaskini na uchochole wa kupindukia.

Kamisheni ya Uchumi na Jamii ya Asia Magharibi (ESCWA) imesema, ongezeko la umaskini katika nchi za Kiarabu litawaathiri watu zaidi ya milioni 130, na kwamba thuluthi moja ya Waarabu wanaishi chini ya mstari wa umaskini.

Ripoti ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imesema kuwa, bara Arabu lilisajili kiwango kikubwa zaidi ya ukosefu wa ajira duniani mwaka uliomalizika wa 2022, la asilimia 12, ikilinganishwa na maeneo mengine.

Novemba mwaka jana pia, Ahmed Aboul Ghait, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) alisema kuwa umaskini umeathiri zaidi ya robo ya jamii katika nchi za Kiarabu.

Kinaya ni kwamba, nchi kadhaa za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia zinaongoza kwa israfu ya chakula duniani. Kwa mujibu wa  jarida la The Economist, Wasaudia wanaongoza kati ya raia wa nchi zote duniani katika israfu ya umwagaji na utupaji mabaki ya chakula.

Aidha baadhi ya tawala za Kiarabu zimekuwa zikikosolewa kwa kutumia mabilioni ya dola katika mambo yasiyo na maana, kama kuagiza silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola kwa ajili kuzitumia katika vita dhidi ya Yemen na mashindano ya kumiliki klabu za soka haswa za Ulaya; huku zikiwapuuza wananchi wa nchi hizo.

Haya yanaripotiwa katika hali ambayo, hivi karibuni, mchezaji mahiri wa soka Cristiano Ronaldo alijiunga na klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia kwa mkataba utakaodumu hadi 2025, na anatazamiwa kupokea mshahara mkubwa zaidi wa kandanda katika historia, wa zaidi ya panu milioni 177 kwa mwaka.

Kadhalika takwimu rasmi zinaonesha kuwa, watu zaidi ya bilioni moja wanateseka kwa baa la njaa na lishe duni katika maeneo mbali mbali duniani.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *