UN: Watu 30,000 wamekimbia ghasia za kikabila nchini Sudan Kusini

Uvamizi wa silaha katika eneo la Sudan Kusini lililokumbwa na mapigano ya kikabila umewalazimisha raia wasiopungua 30,000 kukimbia makazi yao. Hayo yamesemwa leo Alkhamisi na shirika la kukabiliana na hali za dharura la Umoja wa Mataifa na kuhimiza kukomeshwa haraka ghasia hizo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, tarehe 24 mwezi huu wa Disemba, watu wenye silaha kutoka jimbo la Jonglei, la mashariki mwa Sudan Kusini walishambulia raia katika eneo la karibu na Greater Pibor.

Ghasia hizo zimetokea baada ya mapigano ya mwezi uliopita ya kaskazini mwa Sudan Kusini ambayo yalipelekea maelfu ya watu kukimbia makazi yao katika jimbo la Upper Nile.

Sara Beysolow Nyanti, mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu nchini Sudan Kusini amesema: “Watu wameteseka vya kutosha. Raia, hasa wale walioko katika mazingira magumu zaidi – wanawake, watoto, wazee na walemavu – wanabeba mzigo mkubwa wa mgogoro huu wa muda mrefu.”

OCHA imetoa ufafanuzi zaidi kwa kusema: “Takriban watu 5,000 wameomba hifadhi katika mji wa Pibor na kuitaka jamii ya kimataifa ilisaidia shirika hilo kuwahudumia kwa dharura wakimbizi hao.

Mapigano hayo katika jimbo la Upper Nile pia yamewafanya wanavijiji kutafuta hifadhi kwenye vinamasi na maeneo hatarishi ili kusalimisha roho zao na kukwe mapigano ya umwagaji damu, huku kukiwa na ripoti za raia kubakwa, kutekwa nyara na kuuawa.

Mashirika ya kimataifa ikiwa ni pamoja na Timu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) na taasisi ya kikanda ya IGAD yamesema katika taarifa ya pamoja ya leo Alkhamisi kwamba “wana wasiwasi mkubwa” na kuongezeka ghasia huko Sudan Kusini.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *