Maafisa wa shirika moja la misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa wamesema kuwa, wana wasiwasi mkubwa kwamba, zaidi ya watu 500,000 wamekimbia makazi yao ndani na karibu na Goma huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema kuwa hali ya hatari na kuongezeka vitisho vya kiusalama na afya vinavyowakabili watu waliokimbia makazi yao ndani na karibu na Goma vimewatia wasiwasi mkubwa maafisa wa ofisi hiyo.
Taarifa ya OCHA imesema: “Zaidi ya watu 500,000 kwa sasa wanaishi katika maeneo ya wakimbizi kuzunguka jiji hilo baada ya kukimbia mapigano kati ya jeshi la Kongo na makundi yenye silaha katika maeneo ya Masisi na Rutshuru, ya Kivu-Kaskazini.”
Imeongeza kuwa: “Tangu mapema mwezi ulioisha wa Machi, matukio kadhaa ya mashambulizi ya makombora na miripuko iliyotokea ndani na karibu na maeneo ya watu waliokimbia makazi yao huko Goma yameua watu wanane na kujeruhi 34.”
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewataka walinda amani wa timu ya Umoja wa Mataifa inayojulikana kwa jina la MONUSCO kuondoka nchini humo, ikilalamika kuwa haiwalindi raia mbele ya ghasia zilizoenea katika majimbo ya mashariki mwa nchi hiyo.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshaidhinisha kuondoka askari wa MONUSCO na timu hiyo imesema itatii amri ya umoja huo. Tayari timu hiyo iko kwenye mchakato wa kusimamisha kazi zake huko DRC.