UN yakemea hujuma ya Wazayuni dhidi ya Msikiti wa al Aqsa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekemea hujuma zinazofanywa na Wazayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Ni baada ya Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala ghasibu wa Israel kuvamia na kuingia Msikiti wa Al-Aqsa siku ya Jumanne ya jana akiandamana na polisi wa utawala huo huku akiwa amevalia fulana ya kuzuia risasi.

Hatua hiyo ya Ben Gvir imekabiliwa na upinzani mkali wa nchi nyingi duniani. Wapalestina wametangaza kuwa, hujuma za mawaziri wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa ni ukiukaji wa hadhi ya kisheria ya eneo hilo takatifu.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amepinga hujuma ya Waziri wa Usalama wa Ndani mwenye itikadi kali wa Israel, Itamar Ben-Gvir, katika Msikiti wa Al-Aqsa, akisisitiza umuhimu wa kulindwa na kuheshimiwa hadhi ya kihistoria na kisheria ya Quds na Msikiti wa Al-Aqsa.

Farhan Haq Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametangaza ujumbe wa Guterres kuhusu jukumu la Jordan katika kusimamia maeneo matakatifu ya Kiislamu ya Quds tukufu, na kuzitaka pande zote ziepuke hatua zozote zinazoweza kuzidisha mizozo na mapigano huko Quds na maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu.

Wakati huo huo, Itamar Ben-Gvir, Waziri wa “Usalama wa Taifa” wa utawala wa Kizayuni wa Israel, amesema kuwa atauvamia tena Msikiti wa Al-Aqsa.

Msikiti wa Al-Aqsa unajulikana kama nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Palestina wa Quds, na utawala wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo. Hata hivyo kusimama kidete na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala wa Kizayuni na kuufanya ugonge mwamba.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *