UN yapasisha azimio la Russia la kupambana na ubaguzi wa rangi

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio lililopendekezwa na Russia la “kupambana dhidi ya kutukuzwa kwa Unazi, Unazi mamboleo na vitendo vingine vinavyochangia kuongezeka kwa aina za kisasa za ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kimbari, chuki ya wageni na kutovumiliana.”

Azimio hilo limeidhinishwa kwa kura 120 za ndio, kura 50 za kulipinga na nchi 10 hazikupiga kura.

Muswada wa azimio hilo uliandikwa kwa pamoja na nchi kadhaa zikiwemo Syria, Sudan, Guinea, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali Korea Kaskazini, Pakistan, Venezuela, Vietnam na Belarus.

Azimio hilo linaeleza wasiwasi mkubwa kuhusu vitendo vya “kupongeza makundi ya Kinazi, Unazi mamboleo na wanachama wa zamani wa Waffen SS,” kupitia njia ya kujenga majengo ya kumbukumbu zao na kufanya maandamano ya umma kwa ajili ya kuenzi historia ya Nazi.

Waraka huo unatoa wito kwa serikali za nchi mbalimbali “kubuni na kutekeleza mipango ya kitaifa ya kufuta kabisa ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kimbari, chuki dhidi ya wageni na kutovumiliana”.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, katika miaka ya karibuni waandamanaji wenye hasira nchini Marekani na maeneo mengine duniani wameendeleza mkakati wa kuangusha, kuharibu na kuvunja masanamu ya wabaguzi wa rangi. Katika miji mbalimbali ya Marekani waandamanaji wamevunja masanamu kadhaa ya vinara wa ubaguzi wa rangi na biashara ya utumwa ikiwa ni pamoja na sanamu la Christopher Columbus, mzungu kutoka Ulaya aliyedai kuvumbua bara Amerika na sanamu la Edward Colston aliyekuwa mfanyabiashara wa watumwa, katika karne ya 17.

Wanasiasa nchini Marekani walitoa wito wa kuondolewa alama zote zinazowakilisha wakoloni na wamiliki watumwa baada ya maandamano yaliyochochewa na mauaji ya George Floyd.

George Floyd aliuawa Mei 2020 na polisi mzungu, tukio mbalo limetajwa kuwa lilichochewa na fikra na mienendo ya ubaguzi wa rangi.

Wimbi hilo la kuvunjwa masanamu na nembo za ubaguzi wa rangi na utumwa limeshuhudiwa pia katika nchi kadhaa duniani hususan barani Ulaya.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *