UN: Zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makazi yao katika muda wa miezi minne Somalia

Wasomali zaidi ya milioni moja wamekuwa wakimbizi nchini humo katika kipindi cha zaidi ya miezi minne kutokana na ukame, mashambulizi ya wanamgambo wa al Shabaab na mafuriko. Haya yameelezwa na taasisi za misaada ya kibinadamu.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) na Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC) yameeleza kuwa, watu wasiopungua 433,000 wamelazimika kuhama makazi yao kati ya Januari 1 na  Mei 10 mwaka huu.

Vilevile watu zaidi ya 408,000 wamehama makazi yao kutokana na mafuriko yaliyoviathiri baadhi ya vijiji katikati ya Somalia na wengine 312,000 wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na ukame ulioiathiri nchi hiyo miezi kadhaa iliyopita.

Somalia na majirani zake katika eneo la Pembe ya Afrika zikiwemo Ethiopia na Kenya, zimekuwa zikikabiliwa na ukame mkali katika kipindi cha miongo minne ya karibuni baada ya misimu mitano dhaifu ya mvua iliyoharibu mazao ya wakulima na kuuwa mifugo na kusababisha ukosefu wa chakula.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na wawakilishi wa nchi mbalimbali duniani jana Jumatano walikutana New York kukusanya kiasi cha dola bilioni 7 kwa ajili ya kusaidia raia walioathiriwa na ukame na mafuriko katika Pembe ya Afrika.

Ofisi ya Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) wiki jana ilieleza kuwa watu wasiopungua milioni 43.3 wanahitaji misaada ili kunusuru maisha yao katika eneo la Pembe ya Afrika.

Previous Post
Next Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *